MC aliyejirusha ghorofani Dar kuzikwa leo
MWILI wa mshereheshaji, Joel Misesemo aliyekufa kwa kujirusha kutoka ghorofani kwenye Jengo la Darm Makumbusho mkoani Dar es Salaam, unatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni mkoani humo.
Akizungumza jana na gazeti hili kwa njia ya simu, rafiki wa karibu wa familia ya marehemu, Samwel Sasali alisema ibada ya kuaga mwili wa marehemu itafanyika katika Kanisa la Dar es Salaam Pentecoste (DPC) lililopo Kinondoni.
Sasali alisema hakuna taarifa hadi sasa kuhusu sababu za Misesemo kujirusha kutoka ghorofani na taarifa kamili inasubiri ripoti kutoka kwa daktari.
“Sijaonana naye kwa siku kadhaa, lakini mara ya mwisho tuliongea kwenye simu hakuwa na tatizo lolote na hata Jumapili alienda kanisani na alikuwa na watu wanaongea na hakusema wala kuonyesha kama ana tatizo lolote,” alisema rafiki huyo wa Joel.
Kaka wa marehemu, Reuben Misesemo alikaririwa kwenye mitandao ya kijamii akisema familia haifahamu kwa nini ndugu yao aliamua kujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani.
Reuben alisema usiku wa siku ya kuamkia siku ya tukio, Joel alipiga simu kwa baadhi ya ndugu akiwajulia hali.
Alisema ndugu yake alikuwa na mke ila hakubahatika kupata mtoto kwa miaka tisa tangu alipofunga ndoa mwaka 2014.
“Hapo nyuma alipatwa na ugonjwa wa kupooza upande mmoja wa uso, lakini alikuwa akitumia dawa ndani ya wiki nne zilizopita,” alisema Reuben.
Joel alikuwa mshereheshaji wa shughuli mbalimbali zikiwamo harusi, alikuwa mshauri nasaha. Alikuwa maarufu katika mtandao wa kijamii wa Instagram akitumia jina la Mc Joeevents.