Mchakato hadhi maalumu diaspora kukamilika 2024

UHOLANZI; SERIKALI ya Tanzania inatarajia kukamilisha utaratibu wa kuwapatia hadhi maalum Watanzania waishio nje ya nchi, yaani diaspora ifikapo mwaka 2024.

Hayo yamesemwa katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi kwa heshima ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Akifafanua masuala mbalimbali yaliyowasilishwa kupitia risala ya Watanzania iliyosomwa na mwakilishi wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Uholanzi, Sylvana Lubuva, Makamba amesema utekelezaji wa hadhi maalumu unategemea kufanyika kwa mapitio ya baadhi ya sheria za nchi kama ile ya ardhi na uhamiaji, ili kurahisisha utekelezaji wenye tija kwa walengwa, yaani diaspora na kwamba mchakato huo unatajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele kwenye hadhi maalum ni haki ya kurithi au kurithishwa mali kwa diaspora wa Kitanzania aishiye nje ya nchi. Ili kutekeleza hili kuna maeneo ya sheria yetu lazima yabadilishwe, ili watoto wenu wanaoishi huku nje waweze kurithi au kumiliki ardhi,” amesema Waziri Makamba na kuongeza kuwa pia utaratibu wa kulipa visa pindi diaspora wa Tanzania wanaporudi nyumbani.

“Kwenye hadhi maalum, mtaruhusiwa kuja nyumbani na kukaa kwa muda mnaotaka bila malipo ya visa. Lakini kwanza ni lazima sheria yetu ya uhamiaji ipitiwe na kurekebishwa, ili kuruhusu kurudi nyumbani bila kulipishwa visa,” amesisitiza Waziri Makamba.

Baadhi ya masuala mengine yatakayowanufaisha watumiaji wa hadhi maalum ni fursa na motisha mbalimbali za kuwekeza Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

Amesisitiza umuhimu wa kujisajili kwenye mfumo wa Diaspora Digital Hub, ambapo amesema licha ya kusaidia kuwatambua Watanzania waishio nje ya nchi, pia inarahisisha kwa kiasi kikubwa kuwarejesha nchini pindi majanga makubwa yanapotokea maeneo mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi, jumla ya Watanzania wapatao 3,000 wanaishi nchini Uholanzi na maeneo ya karibu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button