Mchakato waiva ujenzi wa barabara Ifakara-Mahenge

WAKALA wa Barabara Tanzania (Tanroads) imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Ifakara hadi Mahenge.

Haya yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Ulanga, Salim Hasham (CCM).

Mbunge alitaka kufahamu ni lini serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Ifakara hadi Mahenge.

Advertisement

Naibu waziri alisema barabara ya Ifakara Kabaoni hadi Mahenge Mjini yenye urefu wa kilometa 55.4 ni sehemu ya barabara ya Ifakara-Mahenge/Lupiro-Malinyi-Kilosa kwa Mpepo-Londo hadi Lumecha yenye urefu wa kilometa 435.

Alisema serikali kupitia Tanroads imeshatangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa ujenzi wa manunuzi ya uhandisi pamoja na fedha (EPC+F).

“Uchambuzi na tathmini ya zabuni za kumpata mkandarasi/mwekezaji atakayetekeleza mradi huu zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa Juni, 2023,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Christine Ishengoma (CCM) alitaka kujua mpango wa serikali wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mzumbe hadi Mgeta.

Akijibu swali hilo, Kasekenya alisema serikali kupitia Tanroads imeendelea kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mzumbe (Sangasanga)-Langali-Luale-Kikeo yenye kilometa 59.16.

Alisema kilomita 13.5 za lami zimejengwa na zimekamilika kwenye maeneo korofi yenye maporomoko na milima mikali.

Naibu waziri alisema serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia barabara upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *