WAZIRI wa Madini, Dk Doto Biteko amesema mchango wa sekta ya madini unazidi kuongezeka na hadi mwaka 2025 wanatarajia kuvuka lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye pato la taifa.
Dk Biteko alisema hayo Ikulu ya Chamwino, Dodoma jana wakati wa kusainiwa mikataba ya kati ya serikali na kampuni tatu za madini kutoka Perth Australia.
Alisema maendeleo ya sekta hiyo si miujiza bali ni matokeo ya namna Rais Samia Suluhu Hassan anavyoilea na kuwaelekeza.
“Ndio maana mheshimiwa Rais hatushangai namba zinapojitetea zenyewe. Ukuaji wa sekta ya madini kwenye mchango wa pato la taifa kwa kipindi kifupi umeongezeka sana.
“Wakati wa mwezi Julai mpaka Septemba mwaka jana sekta ya madini imeshachangia asilimia 9.7. Tumebakiza asilimia 0.3 ili kufikia lengo lililowekwa kitaifa,” alisema Dk Biteko.
Alisema sekta hiyo imeendelea kuwa tegemeo kwenye mauzo ya bidhaa nje ya nchi na hivyo kuingiza fedha za kigeni nchini.
“Miradi hii yote iliyosainiwa leo (jana) italeta mtaji kutoka nje ya nchi unaofikia dola za Marekani milioni 667. Na jambo la maana wakati dunia inahangaika kutafuta madini ya mkakati sie tunasaini mikataba kuchimba madini hayo ya kimkakati,” alisema Dk Biteko.
Alisema wakati akiingia madarakani wachimbaji hao walikuwa wanachangia asilimia 20 kwenye mauzo yote ya madini lakini leo wanachangia asilimia 40.
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Majadiliano kati ya serikali na wawekezaji, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kila mkataba serikali itakuwa na hisa zisizopungua thamani za asilimia 16.
Alitaja kampuni na mikataba iliyosainiwa jana kuwa ni kampuni ya Peak Rare Earth Limited kutoka Australia kuhusu uendeshaji wa mradi wa uchimbaji wa madini adimu Ngwala mkoani Songwe kupitia kampuni mbili za ubia ambazo ni Mamba Minerals Cooperation itahusika na uchimbaji na Mamba refinery Cooperation itakayohusika na uchenjuaji wa madini.
Profesa Kabudi alisema katika kampuni zote hizo mbili serikali ina hisa asilimia 16 isiyofifishwa, Tanzania ikiwa ni nchi pekee Afrika iliyofanikiwa kuingiza aina hiyo ya hisa kwenye mikataba ya madini.
Alitaja kampuni ya Evolution Energy Limited ya Australia itakayohusika na uchimbaji wa madini ya Kinywe Chilalo wilayani Ruangwa mkoani Lindi kupitia kampuni ya ubia ya Kudu Graphite.
“Serikali itakuwa na umiliki wa asilimia 16 ya hisa wakati mwekezaji atakuwa na hisa asilimia 84. Gharama za uwekezaji wa awali katika mradi huo ni dola za Marekani milioni 100 na taarifa za awali za maoteo za mradi huu serikali itapata asilimia 51, mwekezaji asilimia 41,” alieleza.
Profesa Kabudi alisema kampuni ya Ecograf Limited ya Australia itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya Kinywe Epanko wilayani Ulanga mkoani Morogoro kupitia kampuni ya ubia ya Duma ambapo pia serikali itakuwa na hisa asilimia 16.
Alisema gharama za awali za uwekezaji ni dola za Marekani milioni 127.7 na katika maoteo wawekezaji watapata asilimia 49 wakati serikali itapata asilimia 51 ya mgawanyo.
“Mikataba itakayosainiwa leo (jana) ni ya aina tatu ambayo ni mkataba wa makubaliano ya msingi kuhusu umiliki wa mgawanyo wa faida ya kiuchumi, mkataba wa wanahisa na mkataba ni wa Katiba za kampuni za ubia,” alieleza.
Alisema maudhui ya mikataba hiyo ni serikali kuwa na hisa zisizopungua thamani za asilimia 16 ambazo zinaweza kuongezeka zaidi.
Aidha, alisema pia umewekwa utaratibu wa kuhakikisha Watanzania wanashiriki katika nafasi za juu za uongozi wa kampuni ambazo ni Mtendaji Mkuu, Mkuu wa Operesheni, Mkuu wa Fedha, Mkuu wa kitengo cha Manunuzi na Mkuu wa Rasilimaliwatu. Pia ushiriki wa serikali katika uendeshaji wa mradi kupitia maamuzi ya bodi.
Kuhusu mkataba wa kampuni ya Mamba Refinary, imeainisha mkataba wa ujenzi wa kiwanda cha uchanjuaji katika mradi wa Ngwala.