Mchango wa awamu za kiutawala kuendeleza, kukuza Kiswahili Tanzania (1)

LUGHA ya Kiswahili imekua na kufi kia ilivyo sasa kutokana na michango ya watu na wadau mbalimbali wa lugha hii. Miongoni mwa watu hao ni wakoloni wa Kiarabu, Kijerumani na Kiingereza.

Hawa walichangia kwa upande wao maendeleo ya Kiswahili ingawa haikuwa nia yao kukikuza Kiswahili. Kwa mfano, Waingereza licha ya kuendeleza Kiswahili kwa manufaa yao zaidi walitoa mchango mkubwa walipoamua kusanifisha lugha ya Kiswahili katika miaka ya 1930 ambapo lahaja ya Kiunguja ilichaguliwa kuwa lahaja ya msingi katika kusanifisha lugha ya Kiswahili.

Waliamua kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia katika shule za msingi katika nchi zote za Afrika Mashariki. Hii ilikuwa ni hatua muhimu katika makuzi ya lugha ya Kaswahili. Hatua hii ilifungua milango ya waandishi mbalimbali kuandika vitabu vya Kiswahili. Hata hivyo, wapo Watanzania waliokipigania Kiswahili hadi kukifikisha hapa kilipo.

Makala haya yatajikita zaidi katika kuangalia mchango wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kukiendeleza na kukikuza Kiswahili. Harakati za Mwalimu Nyerere kukipigania Kiswahili zilianzia kipindi cha harakati za kupigania Uhuru.

Kwa mfano, chama cha TANU kilipozaliwa mwaka 1954, Katiba yake iliandikwa kwa Kiswahili japo wakoloni hawakutaka katiba hiyo iandikwe kwa Kiswahili. Mwalimu Nyerere akiwa Mwenyekiti wa chama hicho aliona ni vyema katiba ya chama kuandikwa kwa Kiswahili ili Watanzania wote waweze kusoma na kuelewa katiba ya chama chao, aidha katika harakati zake za kupigania uhuru na katika kampeni zake za kunadi sera ya chama cha TANU alitumia lugha ya Kiswahili kuwaelimisha wananchi kuhusu suala la uhuru na kujitawala. Mwaka 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake, hii ilikuwa hatua nyingine muhimu ya kuendeleza na kukikuza Kiswahili.

Ikumbukwe kuwa Kiswahili ndiyo lugha iliyoleta uhuru hasa kwa kuwaunganisha Watanzania na kuleta nguvu na umoja wa kitaifa. Baada ya uhuru kupatikana Serikali ya Mwalimu Nyerere iliendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.

Desemba 10, 1962, Mwalimu Nyerere alihutubia Bunge kwa Kiswahili ikiwa ni mara ya kwanza Kiswahili kutumika Bungeni. Tokea siku hiyo, Kiswahili kilianza kutumika na hivyo kuwa lugha ya mawasiliano Bungeni. Mwaka huohuo Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ilianzishwa. Pamoja na majukumu mengine ya wizara hiyo, pia ilikuwa na kazi ya kuratibu shughuli zote za ukuzaji wa lugha ya kitaifa kwa kutumia maofisa lugha na utamaduni walioko mikoani.

Ni mwaka huo ambapo Waziri wa Elimu aliwaita wataalamu wa lugha na sheria ili kutoa mapendekezo kuhusu lugha ya Kiswahili itumike kama lugha ya sheria. Mwaka uliofuata Februari 12, 1963, Lugha ya Kiswahili ilitangazwa rasmi kuwa lugha ya taifa. Wizara zilianza kutumia Kiswahili katika nyaraka zao na zilihimizwa kutumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Serikali ya Mwalimu Nyerere haikuishia hapo iliendelea kujipanga zaidi kuhakikisha Kiswahili kinajengewa mazingira bora kiendelee kukua.

Aidha, mwaka huohuo 1963, Kamati ya Kufasiri Sheria kwenda katika lugha ya Kiswahili kutoka katika lugha ya Kiingereza iliundwa. Mwaka huo kulikuwa na matukio mengi yanayohusiana na maendeleo ya Kiswahili ambayo serikali ya wakati huo iliyafanya. Mwaka 1963 Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima nayo ilianzishwa (SAMIKISA 2012).

Lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ilikuwa ni kufundisha stadi za kusoma, kuandika na kuhes- abu. Wanafunzi walifundishwa maarifa mapya katika nyanja mbalimbali za maisha kama kilimo bora, afya, ufugaji, chakula bora n.k.

Pamoja na malengo hayo, taasisi hiyo ililenga kufundisha Kiswahili kigumu kwa watumishi wa serikali na kufundisha Kiswahili kiwango cha kidato cha 4-6 na mtumishi aliyefaulu mtihani huo, aliweza kupandishwa cheo. Vilevile, taasisi hiyo iliundwa kwa ajili ya kufundisha Kiswahili kwa wageni na hasa wale wanaokuja kufanya kazi nchini.

Mwaka 1966, Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala ilianzishwa kwa lengo la kutayarisha mihtasari ya masomo ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya taifa. Katika kipindi hicho Kiswahili kilifanywa kuwa somo la lazima kwa watahiniwa wa kidato cha 4 na 6. Jambo lingine la msingi ni kuwa taasisi ilipewa kazi ya kuteua vitabu vya kusoma vya somo la fasihi ambavyo vitatumika katika kuwataini wanafunzi. Mpaka kufikia mwaka 1966, Kiswahili kilishapiga hatua kubwa kuelekea katika mafanikio ya kukua na kuongeza idadi ya wazungumzaji na ilikwishatangazwa kuwa lugha ya taifa.

Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere, iliona ni vyema lugha hii iwe na chombo kitakachosimamia maendeleo yake. Ndipo mwaka 1967, serikali iliamua kuunda baraza la kuratibu na kusimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili yaani Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), ambalo lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge ya mwaka 1967 Na. 27. Pamoja na majukumu mengi mengine, jukumu kuu la Bakita ni kuratibu na kusimamia maendeleo na matumizi sanifu na fasaha ya Kiswahili.

Kuhimiza matumizi ya Kiswahili sanifu katika shughuli rasmi na za kawaida nchini. Hatua mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa na serikali ili kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inazidi kukua na kuendelea kushamiri nchini. Mwaka 1968, Kiswahili kilifanywa rasmi kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi kuanzia darasa la 1 hadi 7. Aidha, Kiswahili kilifanywa kuwa lugha ya kufundishia katika vyuo vya elimu daraja la A na C.

Katika kipindi hiki Kiswahili kilifanywa kuwa lugha ya shughuli za taifa. Pia, serikali iliamua ifundishe masomo ya siasa, Kiswahili na elimu ya kujitegemea. Haya yote yalifanyika kwa ajili ya kukuza Kiswahili. Mwaka 1971, jambo la msingi sana lilifanyika, serikali iliamua kuanzisha Baraza la Mitihani la Taifa kwa ajili ya kutunga mitihani mbalimbali ikiwamo ya somo la Kiswahili. Ikumbukwe kuwa mpaka kufikia mwaka huo, Kiswahili kilifanywa kuwa somo muhimu la kutahiniwa. Mwaka huohuo, Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ilianzishwa ambapo iliendelea kurusha matangazo yake kwa Kiswahili.

Redio hiyo ilikuwa ikirusha vipindi vya elimu kwa umma kwa lugha ya Kiswahili. Mwaka huo pia gazeti la Uhuru lilianzishwa, habari ziliandikwa kwa Kiswahili na wananchi wengi walisoma makala zilizoelimisha umma.

 

Kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Kwanza pamoja na wadau wengine, mwaka 1987, Julai wakuu wa nchi za Afrika katika kikao chao cha mwaka huo, kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia, waliamua Kiswahili kitumike katika vikao vyao vya Umoja wa Afrika (AU).

Baadaye mwaka 2004, Julai, Kiswahili kilianza kutumika rasmi kwenye mikutano ya wakuu wa nchi. Aidha, Kiswahili kilipendekezwa kitumike katika vikao vya baadhi ya mashirika ya AU. Juhudi za kukuza Kiswahili, hazikuishia hapo, awamu nyingine pia zimefanya kazi kubwa za kukuza Kiswahili. Ili kujua ni juhudi gani zikifanywa na awamu zilizofuata, makala nyingine zitakazofuata zitaelezea hayo. Itaendelea wiki ijayo.

Tujivunie na Kukienzi Kiswahili, Moja ya Tunu za Taifa Letu. Mwandishi wa makala haya ni Mchunguzi Lugha Mwandamizi kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA),

simu: 0683 680556.

Habari Zifananazo

Back to top button