WINGU la huzuni lilitanda anga la nchi ya Tanzania wakati Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (wakati huo) alipoutangazia umma wa Watanzania kifo cha Rais Dk John Pombe Magufuli.
Haikuwa rahisi hasa kutokana na ukweli kwamba, katika historia ya Tanzania, tangu uhuru hakukuwahi kutokea kifo cha Rais aliye madarakani. Hofu, mashaka, wasiwasi ilikuwa sehemu ya maisha ya Watanzania lilipotokea tukio hilo.
Leo Machi 17, 2023 ni kumbukizi ya miaka miwili sasa ya kifo cha Dk Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano, aliyezoeleka kuitwa JPM ikiwa ni kifupi cha jina lake.
Enzi ya uhai wake, ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa mambo ambayo Dk Magufuli aliyasimamia kwa nguvu zake zote na kufanya sasa Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zinazoheshimika na kutambuliwa ulimwenguni ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumiaji wake kutoka katika nchi mbalimbali.
Dk Magufuli hakusita kuonesha waziwazi utashi wake wa kuikuza lugha hii hasa wakati wa mikutano mbalimbali ya ndani ya nchi na hata katika mikutano aliyoifanya na viongozi wa mataifa ya nje ambapo alidiriki kuongea kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Ni Dk Magufuli ambaye aliwashawishi viongozi wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kukubali Kiswahili kutumika katika mawasiliano ya jumuiya hiyo ambapo wakuu hao walilipitisha wazo hilo bila kupingwa na sasa lugha ya Kiswahili inatumika katika mikutano ya nchi 16 wanachama wa SADC.
Aidha, mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili hakuweza kuyaficha hasa pale alipofanya ziara katika nchi mbalimbali hasa za Kusini mwa Afrika ambapo alidiriki kuwapatia vitabu vya Kiswahili baadhi ya marais. Alitoa vitabu kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ili ajifunze Kiswahili ambapo naye kwa kuonesha kulikubali wazo la Dk Magufuli alisema nchi yake itaanza kufundisha Kiswahili katika shule za msingi na sekondari.
Katika kusisitiza utashi wake wa dhati kuhusu kueneza lugha ya Kiswahili, Dk Magufuli pia aliwahi kuwapatia zawadi ya vitabu vya Kiswahili wakuu wa nchi zote za SADC wakati wa mkutano wao wa 39 uliofanyika jijini Dar es Salaam ili waende navyo nchini mwao kwa ajili ya kujifunza lugha hiyo.
Wakati wa kukabidhi uenyekiti wa SADC kwenye mkutano wa 40, Dk Magufuli katika hotuba yake alisema: “Ni imani yangu kuwa kuridhiwa kwa lugha hii ya kwanza ya Kiafrika kwenye jumuiya yetu, kutachochea ushirikiano na utengamano ndani ya jumuiya, na hii ndiyo sababu nimeamua kutoa hotuba yangu kwa Kiswahili na nimefarijika kuona kuwa, wengi wenu mnanisikiliza bila kutumia vifaa vya kukalimani lugha. Hii inaonesha kuwa mnaifahamu na kuielewa vyema lugha ya hii adhimu ya Kiswahili.”
Pia, msukumo uliooneshwa na Dk Magufuli katika kuikuza, kuiendeleza na kuieneza lugha ya Kiswahili kumeifanya lugha hii kukubaliwa kuwa miongoni mwa lugha za mawasiliano zitakazotumika katika Umoja wa Nchi Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika (ADPA).
Mchango wa Dk Magufuli katika maendeleo ya Kiswahili ni mkubwa sana kwani mbali na kuitambulisha lugha hii kimataifa, aliweza kukuza fasihi ya Kiswahili, kukuza msamiati, kuongeza fursa za ajira kwa wataalamu wa Kiswahili, kuwatia ari wakalimani na wafasiri na kuwahimiza wananchi kuthamini matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.
Aidha, Dk Magufuli alisisitiza lugha ya Kiswahili kutumika katika maandiko ya sheria, mahakamani, katika taasisi za umma na sehemu nyingine ambapo kwa kuonesha dhamira yake ya kweli katika matumizi ya Kiswahili aliweza kumpandisha cheo Jaji Zepharine Nyalugenda Galeba kutoka kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kutokana na kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili.
Pia, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuendeleza na kuikuza lugha ya Kiswahili, ambapo hivi karibuni katika mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, Samia alihutubia kwa lugha ya Kiswahili.
Katika mkutano huo Rais Samia aliwashukuru wakuu wa nchi na serikali kwa kupitisha Azimio la Kiswahili ambapo hivi sasa Kiswahili ni lugha rasmi ya mawasiliano katika umoja huo.
Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inathamini matumizi ya Kiswahili, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na ya Bunge kwa 2021/22, alisisitiza kwamba serikali itatekeleza mambo muhimu ikiwemo kuenzi lugha ya Kiswahili.
Hakika, Dk Magufuli atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili, kwani aliweza kukivusha nje ya mipaka ya Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na dunia nzima.
Watanzania tuna kila sababu ya kusema endelea kupumzika pema Dk John Pombe Joseph Magufuli kwani kazi ulioifanya ni njema. Ulikitendea haki Kiswahili na sasa kazi hiyo inaendelea kwani Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza lugha hii adhimu ya Kiswahili.
*Mwandishi wa makala haya ni Mfasiri Mwandamizi kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), simu: 0754 566548.