MCHINJITA :Serikali ilete suluhisho la kuduma barabara Kibiti -Lindi

DAR ES SALAAM: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita ameishauri serikali kuleta suluhisho la haraka na kudumu kuhusu ujenzi wa barabara ya Kibiti-Lindi.
Aidha, Mchinjita ameshauri kufanyika upembuzi yakinifu wa makaravati yote yanayokatiza mabonde ya mto Matandu na Mbwemkuru ili kujenga madaraja yenye uwezo wa kuhimili kiwango cha maji yanayopita .
“Barabara ya kusini kibiti Lindi inapaswa kujengwa upya . Barabara ilijengwa chini ya kiwango na imeharibika yote. Masuluhisho yanayotekelezwa sasa ya kurekebisha vipande vipande hayatoondosha msingi wa tatizo,” amesema Mchinjita.
Katika taarifa yake fupi aliyoitoa leo Aprili 17, Mchinjita ameshauri serikali ihakikishe inaleta usafiri wa uhakika wa meli/boti iendayo kasi kati ya Dar es salaam na mikoa ya kusini.
Mchinjita amezungumza hayo baada ya mawasiliano ya barabara kuu ya Dar es salaam -Lindi kukatika eneo la Somanga kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.



