MCHUNGAJI wa Kanisa la KKKT Makedonia Lubaga, Manispaa ya Shinyanga, Harold Gamalieli Mkaro, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga na kusomewa shitaka la kujaribu kulawiti mtoto wa miaka 8.
Mchungaji huyo alifutiwa kesi ya awali namba 107, Agosti 24, 2022 na Jamhuri katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, kwa sababu za kisheria, lakini alikamatwa tena na kurejeshwa mahabusu, hadi leo alipofikishwa mahakamani tena.
Akisomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Marry Mrio, mshitakiwa huyo amekana shitaka hilo.
Mwendesha Mashitaka wa Jamhuri, alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo la kujaribu kulawiti mtoto huyo wa miaka 8, Agosti 12, 2022, eneo lilipo kanisa hilo Makedonia Lubaga, kinyume na kifungu cha 155 cha kanuni ya adhabu, sheria namba 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2019.
Mwendesha Mashtaka upande wa Jamhuri, Jukael Jairo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekalimika na wako tayari kusoma hoja za awali na kusikiliza kesi hiyo.
Kwa upande wake wakili wa utetezi, Jeofrey Tuli aliiomba mahakama hiyo, ahirisho kutokana na mteja wake kutokuwa sawa kisaikolojia, baada ya kukaa mahabusu siku tano.
Wakili Tuli akaomba mteja wake kupewa dhamana, ambapo upande wa mashitaka haukuwa na kipingamizi.
Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Marry Mrio alimtaka mshitakiwa kuwa na bondi ya Sh milioni 3, pamoja na wadhamini wawili wenye kiasi hicho hicho cha fedha na mali isiyohamishika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho, ambapo mahakama hiyo itaanza kuwasikiliza mashahidi sita kutoka upande wa Jamahuri na mshitakiwa amerudishwa rumande.