WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo anamwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika (APSD) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia Oktoba 4 hadi 6.
Mdahalo huo unawakutanisha Viongozi wa Ngazi za juu wa Serikali wa Afrika, Watendaji wa Taasisi mbalimbali, Wanazuoni na Watunga Sera kwa lengo la kujadili na shughulikia changamoto za Amani na Usalama zinazoendelea sehemu mbalimbali barani Afrika.
SOMA: Balozi Mahmoud aapishwa ubunge
Aidha mdahalo huo unalenga kuongeza uelewa wa kina kuhusu changamoto hizo na kuhamasisha mijadala yenye tija itakayoleta suluhisho la migogoro hiyo kwa kuzingatia muktadha na maslahi ya bara la Afrika.
Mdahalo huo unaoongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuelekea Afrika yenye Amani na Usalama: Changamoto na Fursa” utajikita zaidi katika kujadili migogoro ya kisiasa inayoendelea Sudan, baadhi ya nchi za Ukanda wa Afrika Magharibi na Pembe ya Afrika ikiwa ni maeneo ambayo yamekumbwa na changamoto hizo zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Taasisi ya Thabo Mbeki ilianzishwa mwaka 2010 kwa madhumuni ya kuibua na kendesha midahalo na mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali barani Afrika, kufanya tafiti na uchambuzi wa Sera, kuhimiza ubia na ushirikiano katika masuala ya maendeleo Afrika, kuwawezesha Wanawake na Vijana katika kuhifadhi na kutangaza historia na utamaduni wa Afrika.
Ili kufikia adhma hiyo, pamoja na masuala mengine Taasisi ya Thabo Mbeki inatekeleza mipango mbalimbali ikiwemo ya Umoja wa Afrika na Kimataifa, kama vile Mfumo wa Kujitathmini wa Utawala Bora wa Afrika (APRM), Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, Mapango wa Uwezeshaji Wanawake wa Afrika na Mdahalo wa Umoja wa Vijana Afrika (the Pan-African Youth Dialogue).
Mbali na kushiriki mdahalo huo Balozi Kombo atafanya mazungumzo ya uwili na Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Ronald Ozzy Lamola na Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Afrika Kusini(ANC), Fikile Mbalula.