MIAMI, Marekani: KOCHA wa timu ya Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Marekani (MLS), Gerardo Tata Martino amesema mchezaji wake Lionel Messi ataikosa mechi ijayo ya Jumamosi dhidi ya DC United kutokana na majeraha aliyoyapata sehemu ya paja la mguu wake wa kulia.
Huo utakuwa ni mchezo wa kuukosa baada ya kupumzishwa katika mchezo wa kwanza waliopoteza kwa mabao 3-2 Jumapili iliyopita dhidi ya Montreal.
Kocha Martino amesema Messi ataukosa mchezo huo wa pili katika Ligi ya MLS baada ya kupata majeraha ya mguu wake wa kulia ndiyo maana alimtoa nje ya uwanja ili asipate majereha zaidi katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa ya CONCACAF ambapo waliishinda timu ya Nashville kwa bao 3-1.
“Messi alionekana kuwa na changamoto kwenye msuli wake wa kulia, tuliona asingeweza kuendelea kucheza kwa muda mrefu sababu alionekana akisumbuliwa na hali hiyo ndipo tukaamua kumtoa na anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi ili kufahamu ukubwa wa jereha alilonalo kwa ajili ya matibabu,” Martino amesema
Messi anatarajiwa kurejea katika timu ya taifa la Argentina kwa ajili ya mechi za FIFA baada ya mapumziko ya Ligi ya MLS huku Inter Miami ikijipanga kuikabili Monterrey robo fainali ya CONCACAF.