Meya aagiza viongozi kupima maeneo ya masoko

MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe ameagiza viongozi wa jiji hilo waoneshe, wapime na kutambulisha maeneo ya masoko katika jiji hilo.

Mwamfupe alisema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wakati wakijadili masuala yanayohusu maendeleo ya jiji hilo.

Profesa Mwamfupe alisema, Jiji la Dodoma linatakiwa kuonesha maeneo yote katika kata 41 za jiji hilo.

Alisema jiji hilo linatakiwa kutangulia katika kuonesha maeneo hayo na kuweka alama ili maeneo hayo yasivamiwe na kuingiliwa na watu kwa kufanya matumizi ikiwamo kujenga makazi.

Meya huyo wa Jiji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Madukani, alisema haipendezi wananchi kutangulia kuonesha maeneo ambayo jiji linayajua na yapo kwenye ramani.

Awali ya Diwani wa Kata ya Makole, Omar Haji alilalamika kwamba baada ya wafanyabiashara ndogo ndogo kuondolewa katika soko la Sabasaba eneo hilo la katikati halitumiki ipasavyo.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Makole ambako Jiji la Dodoma limewekeza lakini halijatengeneza vizuri miundombinu kwa ajili ya wafanyabiashara wakiwemo wa mboga kuhamia katika hapo.

Habari Zifananazo

Back to top button