Mfuko waja na mikopo ya nishati safi

DODOMA: KATIKA kuunga jitihada za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini, Mfuko wa Self MF umeanzisha bidhaa mpya ambapo wanatoa mikopo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na nishati mbadala, nishati safi sambamba na kuuza bidhaa za gesi na vifaa vyake.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mfuko huo wa Kanda ya Kati Dodoma na Singida Aristid Tesha akisema kuwa lengo lao ni kutimiza nia ya serikali ya kupunguza matumizi ya mkaa na kuni kwa wananchi.

“Hawa wanaofanya nishati mbadala tumewalenga na tunawapa mkopo wenye riba nafuu ili waweze kupanua wigo kufanya shughuli zao na kuweza kuwafikia wananchi,” alisema meneja huyo.

Kwa kuongezea alisema kuwa kwenye nishati mbadala wamejikita kwa wanaosambaza sola za umeme waliopo vijijini na mijini wanaowauzia wananchi kwa bei nafuu.

Aidha akizungumzia mikopo ya watumishi wa umma alisema kuwa wanatoa mikopo kwa watumishi kupitia mishahara yao ambapo huduma ya mikopo hiyo inapatikana katika  matawi yaliyopo mikoa 12 huku akiwahimiza wananchi kutembelea banda la Self MF ili waweze kupata maelezo ya huduma mbalimbali zinazotolewa na mfuko huo.

Naye Meneja Rasilimaliwatu na Utawala Johari Magara alieleza kuwa lengo kuu la kushiriki maadhimisho hayo ni kuwapa taarifa wananchi ya huduma za mikopo zinatolewa na mfuko huo.

Mfuko wa self MF ulianza rasmi 2014 ambapo lengo kuu ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye unafuu.

Mfuko huo unatoa mikopo mbalimbali ikiwemo mikopo ya watumishi wa umma, wafanyabisahara, wajasiriamali wadogo na wa kati, mikopo ya wakulima, mkopo wa wazabuni pamoja na Nishati safi.

Alieleza kuwa mbali na mikopo hiyo pia mfuko huo unatoa mkopo wa bima za gari,nyumba, za wizi na nyingine zote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button