Mfumo PPP utumike kuokoa fedha za umma

DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Mwanga,Joseph Tadayo amezishauri kampuni, taasisi na mashirika ya umma kuingia katika mfumo wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) ili waweze kujiendesha kwa faida na kuongeza tija kwa umma .

Akichangia Taarifa  ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) inayojadiliwa bungeni mjini  Dodoma,Tadayo amesema sheria ya ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ( PPP) imeweza kuleta  tija kwa baadhi ya makampuni, taasisi za serikali na mashirika ya umma nchini yaliyokuwa yakijiendesha kihasara.

“sasa tunapopata hasara tunakuwa na mambo matatu  labda tukakope ili tuongeze mitaji,la pili serikali ikusanye kodi kwa wananchi halafu iwape wao wafanye biashara,lakini la tatu kuingia katika utaratibu kama huu wa PPP,” amesema.

Advertisement

Aliongezea,”Wakati wa kurekebisha mashirika ya umma katika serikali ya awamu ya tatu  yapo makampuni na taasisi za serikali yaliyoingia katika mfumo wa PPP na yalionyesha mafanikio makubwa,  hatuna kelele zozote Kampuni ya Bia Tanzania -TBL, hatuna kelele Kampuni ya Sigara, hatuna kelele NMB na mashirika mengine yaliingia kwenye utaratibu huu yameweza kufanikiwa”, Tadayo  alimalizia.

Hatahivyo , Tadayo amewashauri viongozi wa makampuni, taasisi na mashirika ya umma kuanza kutumia ubunifu wa uendeshaji wa shughuli zao ili kuondokana na hasara za upotevu wa fedha za umma.

“Makampuni mengi ya umma yapo  ambayo yamefanya vizuri lakini yapo mengine bado yanajiendesha kihasara , kila mwaka tunasikia TTCL imepata hasara hasara  , NARCO imepata hasara , NBC imepata hasara ,ATCL na makampuni mengine kunahaja ya kuboresha mifumo ya uendeshaji,” alisema Tadayo.

SOMAKamati yaikumbusha TTCL kuhusu gawio

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeonyesha kuwa miongoni mwa makampuni ambayo yanaongoza kujiendesha kihasara ni Kampuni ya Simu Tanzania TTCL ambayo kila mwaka inajiendesha kwa hasara jambo ambalo wametakiwa kuwa na utaratibu mwingine wa kujiendesha utakaowasaidia kujiendesha kwa faida na kukabiliana  na soko la biashara ya mawasiliano nchini.