Kamati yaikumbusha TTCL kuhusu gawio
KAMATI ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema licha ya changamoto ilizonazo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ila linapaswa kutoa gawio kwa serikali pindi muda wa kufanya hivyo utakapofika.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwanaisha Khamisi Juma amesema hayo leo Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipotembeleà shirika hilo kuona wanavyofanya kazi kama sehemu ya taasisi za Muungano.
Akizungumzia utendaji wa shirika hilo, mwenyekiti huyo amesema kamati imeridhika na kinachofanywa na shirika hilo pamoja na jitihada zinzofanywa na marais wote kwa kuhakikisha wanawekeza miundombinu imara.
Hata hivyo amelitaka shirika hilo kutatua changamoto zinazowakumba ikiwemo suala zima la deni.
SOMA: Serikali yashauriwa kutafuta mwekezaji TTCL
Amesema pamoja na mambo mengine waliyojadiliana wamewashauri kukaa pamoja Ili kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikumba shirika hilo kwani ni mambo ya kimuungano.
“Pamoja na mengi mazuri yaliyofanywa na shirika hili lakini kwenye mafanikio hakukosi changamoto hivyo wakae pamoja ili kuzitafutia Suluhu,”amesema Mwenyekiti Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo bila kufafanua zaidi kuhusu deni.
Mkurugenzi wa TTCL, Moremi Marwa amesema wamepata maelekezo na watayafanyia kazi kama inavyostahili.
Mbali ya majadiliano hayo, kamati hiyo imetembelea kituo cha uangalizi na uendeshaji wa mtandao na miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.