Mgunda alia na washambuliaji Simba

KOCHA Mkuu wa Simba Juma Mgunda amesema licha ya ushindi walioupata juzi dhidi ya Ihefu FC,  lakini bado ana kazi kubwa ya kurekebisha safu yake ya ushambuliaji, ambayo imekuwa ikipoteza nafasi nyingi wanazo tengeneza.

Simba juzi iliibuka na ushindi wa bao 1-0, na kupanda nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini sasa imeshuka hadi ya tatu baada ya Yanga kushinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar jana.

Akizungumza na baada ya mchezo, kocha huyo ameeleza kuwa ubutu wa safu yake ya ushambuliaji umekuwa ni tatizo linalojirudia mara kwa mara hivyo hivyo mipango yake ni kuhakikisha analifanyia kazi hilo kabla ya kuanza mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika .

“Nianze kuwapongeza vijana wangu kwa kupambana na kupata pointi tatu sababu hii ni ligi na timu zote zimejiandaa hata hawa Ihefu pamoja na kwamba wapo chini kwenye msimamo lakini siyo timu dhaifu ni matokeo tu hayajakaa upande wao lakini tatizo linalotukabili ni kushindwa kuzitumia vizuri nafasi tunazotengeneza,”.

“Nimekuwa nikilifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi na nitaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na wenzangu mpaka kuhakikisha tatizo hilo linamalizika sababu kadri tunavyokwenda ugumu unaongezeka na mbaya zaidi tupo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa,” alisema Mgunda.

Kocha huyo ameeleza kuwa katika mchezo huo walitumia mifumo tofauti kulingana na uchezaji wa wapinzani wao Ihefu lakini zote zilionekana kufeli hasa baada ya washambuliaji wake Moses Phiri na Habibu Kyombo kushindwa kuzitumia vizuri nafasi walizopata.

Mgunda alisema pamoja na yote, lakini mashabiki wao hawapaswi kuvunjika moyo bali wanatakiwa kuendelea kuwapa sapoti na kuwa na uvimilivu katika kipindi hiki kigumu huku yeye na wenzake wakipambana kuhakikisha hali hiyo inaondoka.

Naye Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Juma Mwambusi alisema sababu ya kupoteza mchezo huo ni makossa madogo yaliyofanywa na safu yake ya ulinzi lakini vijana wake walifanya kazi kubwa kwa dakika zote 90.

Mwambusi ameeleza kuwa kufeli kwa mipango yao kipindi cha pili ndiko kuliko wapa Simba bao hilo lakini wamekubali matokeo na wanarudi kujipanga ili kufanya vizuri kwenye mechi zinazo fuata.

“Kama isingekuwa makosa madogo yaliyofanywa na kipa wetu basi tungeweza kupata hata pointi moja kama siyo tatu vijana wangu walicheza vizuri na kuziba njia zote ambazo Simba walikuwa wanazitumia lakini pamoja na kupoteza nafurahi kuona kiwango cha timu yangu kimeendelea kuimarika siku baada ya siku,” alisema Mwambusi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button