NAIBU Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Dk Festo J. Dugange, amemsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa Wilaya ya Bunda, Timothy Mwajara na amewataka Mkurungenzi, Changwa Mkwazo na Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo Jamaly Kimamba kujitathimini utendaji kazi wao kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Bunda.
Ametoa maelekezo hayo leo Januari 13, 2023, wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya Bunda, ambapo hajaridhishwa na kasi ya ujenzi na thamani ya fedha zilizotumika katika ujenzi ambao unaendelea, ambapo mpaka sasa umegharimu Sh bilioni 3.6.
Amesema Mhandisi wa Wilaya ya Bunda ana mwaka mmoja tangu ameletwa katika halmashauri hiyo, lakini ameshindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa majengo ya Hospitali hiyo na kamuagiza Katibu Tawala Mkoa, kuleta Mhandisi mwingine atakayeweza kusimamia ujenzi wa hospitali hiyo.
Amemtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri kujitafakari utendaji kazi wake, ambapo ana miezi sita tangu ameletwa katika halmashauri hiyo, lakini haoneshi ufanisi wa kazi yake ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ambao umeanza tangu mwaka 2019.
Amesema wakati akikagua hospitali hiyo ameona kuna vifaa ambavyo vimenunuliwa tangu mwaka 2019, kama madirisha ya aluminium, milango, vigae na mbao lakini hayajafungwa katika maeneo yake na kusababisha kuharibika na vingine kuibwa.
Amesema tangu Mei mwaka 2019, serikali ilitoa Sh bilioni 1.8, kujenga majengo saba ya awali, lakini mpaka sasa hayajakamilika kwa sababu watendaji waliosimamia ujenzi walifanya ubadhirifu wa fedha na walishindwa kusimamia.
Ameagiza kupatiwa majina watumishi wote, ambao walihusika katika usimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo ambao wamehamishiwa maeno mengine ikiwa ni pamoja waganga wakuu, wahandisi, maofisa ununuzi na watumishi wengine, ili waweze kurudi kujibu tuhuma na kuchukuliwa hatua sitahiki.
Amemtaka Mkurugenzi na menejimenti yake kujitafakari juu ya utendaji kazi wao katika usimamizi wa fedha za miradi ambazo zinaletwa katika halmashauri hiyo, lakini hazisimamiwi na hazitumiki wala kufanya kazi halisi inayopaswa kufanyika.
Ameagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na TAKUKURU kuchunguza thamani ya fedha iliyotumika kama inaendana na kazi iliyofanyika mpaka sasa na tuhuma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wizi ambao umekuwa ukifanyika mara kwa mara, ili wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua sitahiki.