Miaka minne ya nguvu

SERIKALI ya Awamu ya Sita imepata mafanikio katika kuboresha huduma za jamii zikiwamo za afya, elimu, maji na kupunguza kiwango cha umasikini.

Leo serikali hiyo inatimiza miaka minne kwa kuwa kiongozi wake mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan aliapishwa Machi 19, 2021 katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, Machi 8, mwaka huu, Rais Samia alisema serikali imepiga hatua kupunguza umasikini.

“Mpaka tunafanya tathmini ya mpango wa tatu wa maendeleo tayari tulishapunguza umaskini kwa kiwango cha asilimia 26 kutoka kiwango tulichokuwa tunaanza utekelezaji na hii ilikuwa 2015,” alisema Rais Samia.

Aliongeza: “Kitaifa tumeshaondoa njaa kwa asilimia 100, na katika lengo la kujitegemea kwa chakula tunajitegemea  kwa chakula kwa asilimia 128, sasa kilichobaki ni kwa mtu mmoja mmoja na jitihada za kuhakikisha habaki na njaa”.

Rais Samia alisema katika sherehe hizo jijini Arusha kuwa Tanzania imeendelea kupiga hatua katika sekta ya afya hasa katika kuongeza miundombinu na vifaatiba.

“Mnatambua serikali yenu imejitahidi kujenga miundombinu ya afya nchini nzima kuanzia zahanati, hospitali za kata, wilaya, mkoa na rufaa pamoja na vifaa vya matibabu,” alisema mkuu wa nchi.

Rais Samia alisema huduma za afya kwa mama na mtoto zimeimarika kwa kupunguza idadi ya vifo vya wanawake wakati wa kujifugua.

“Tumeweza kupunguza vifo vya wanawake wakati wa kujifungua vifo vya wanawake wa Tanzania vilikuwa vifo 1,500 kwa vizazi hai 100,000 leo tunapozungumza ni vifo 104 kwa vizazi hai 100,000 vilevile tumepunguza vifo kwa watoto,” alieleza.

Katika sekta ya elimu, Rais Samia alisema kwa sasa idadi ya wanafunzi imefikia sawa kwa sawa baina ya wavulana na wasichana.

Alisema kwa sasa usawa wa kijinsia umeongezeka katika wanafunzi wanaosailiwa kwa shule za msingi na sekondari kwa 2025 na wanafunzi wanaodahiliwa katika vyuo vikuu na vyuo vya ufundi umeongezeka na wasichana nao idadi yao inaongezeka.

Kuhusu usawa wa kijinsia, Rais Samia alisema mwanzoni hali ya usawa wa kijinsia haikuwa ya kuridhisha sana lakini kwa sasa nchi imepiga hatua huku sekta binafsi ikionesha mwanga wa kuwa na wanawake katika nafasi za juu za uamuzi.

Katika sekta ya maji, alisema Tanzania imefikia mafanikio ya maendeleo endelevu ikitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020–2025 kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.

“Ilani ya Uchaguzi ilituelekeza kwamba kwa vijijini twende asilimia 85 na mjini twende asilimia 95, mpaka Desemba mwaka jana vijijini kwa wastani tunakaribia asilimia 80 na mijini kumefika asilimia 90, lakini kuna miradi zaidi ya 1,000 iko nchi nzima ikikamilika tunakwenda kufikia au kupita asilimia tulizotumwa na chama,” alibainisha Rais Samia.

Kuhusu nishati, alisema Tanzania imesambaza umeme vijijini na sasa inatoka kwenye matumizi ya nishati chafu.

Kwenye miundombinu, alisema serikali imejenga njia za usafiri na kurahisisha usafirishaji na inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa wanawake na vijana.

Aidha, alisema serikali imeendelea kupunguza pengo la usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume kupitia marekebisho ya sera, sheria na mikakati ya kukuza uchumi ili kupunguaza pengo la usawa wa jinsia.

Mkazi wa Kijiji cha Kemondo wilayani Bukoba mkoani Kagera, Abbas Omary ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuziimarisha sekta zote. Omary alitoa mfano kuwa sekta ya elimu imeboreshwa kwa kuwa shule zimejengwa na hata zilizokuwepo zimeboreshwa.

“Lakini pia serikali imekuwa na mwendelezo wa kuajiri walimu wa kutosha na wa zamani kupandishwa vyeo kila mwaka lengo kuu ni kuongeza ubora wa elimu kwa jamii na kuleta maendeleo na zaidi kuingia kwenye soko la ushindani katika elimu,” alisema mwananchi huyo.

Mkazi wa Kijiji cha Ibondo wilayani Sengerema, Edward Lushanga alisema Rais Samia ametambua umuhimu wa viongozi wa ngazi za kata na vijiji kwa kuwapatia usafiri unaorahisisha ufanyaji wa shughuli kwani walikuwa wakitembea kwa miguu.

Aidha, Lushanga alisema anajivunia kipindi cha miaka minne ya Samia kwa sababu ametambua na kuonesha thamani ya zao la kahawa.

“Rais Samia amekuwa akihakikisha pembejeo zinapatikana tena kwa bei nafuu na kuhakikisha zao hili linauzwa kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kupitia mfumo wa ushirika ambao unasaidia kusimamia bei na kutomlalia mfanyabiashara wa kahawa, kwani hiyo ndiyo ajenda kuu ya Wizara ya Kilimo iliyopigiwa kelele kwa muda mrefu,” alisema Lushanga.

Wakili wa Kujitegemea, Faudhia Mustapher anayeishi Kaloleni mkoani Arusha, alisema katika miaka minne sekta ya afya imeimarishwa na kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.

Mustapher alisema wananchi mkoani Arusha wana matarajio na imani Rais Samia atafanya mambo makubwa zaidi akichaguliwa kuendelea kuingoza nchi.

“Taifa linamhitaji na wananchi wana imani naye, hivyo ni wajibu wake kuendeleza pale alipoishia kwa maslahi ya taifa, chama na serikali yake kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za nchi yao,” alisema wakili huyo.

Mkazi wa Daraja Mbili pia jijini Arusha, Hemed Shabir alisema katika kipindi cha miaka minne madarakani Rais Samia amewaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja.

Mkazi wa Longido mkoani Arusha, Solomoni Lekui alisema katika miaka minne Rais Samia amefanya mambo makubwa katika sekta karibu zote.

Mamalishe Hilda Takuru na Tausi Swalehe wamesema katika miaka minne Rais Samia amewainua wanawake kiuchumi ikiwamo fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Wakazi wa Pasua katika Manispaa ya Moshi, Rahma Sabuni na Renatha Mbise wameishukuru serikali kuboresha taratibu za mikopo ya asilimia 10.

Mkazi mwingine wa Pasua, Naomi Fredy amempongeza Rais Samia kwa juhudi za kukuza na kuendeleza usawa wa kijinsia.

Mkazi wa Mtaa wa Negamsi wilayani Babati, Morris Ambosi amempongeza Rais Samia kwa kudumisha amani na utulivu nchini.

Mjasiriamali wa matunda, Lea Salema alimpongeza Rais Samia kwa kuboresha huduma za afya ikiwamo kujenga miundombinu ya hospitali kwa ngazi mbalimbali na kumuomba aendelee kuboresha nishati mbadala ya gesi vijijini.

Mkazi wa Kivule Wilaya ya Temeke, Mwanaidi Ramadhan amempongeza Rais Samia kwa kutumia falsafa ya ‘4R’ kubadilisha siasa za Tanzania.

“Kwa sasa mikutano inafanyika bila ugomvi kati ya polisi na wanasiasa na hili ni jambo ambalo limeipa nchi heshima kubwa kwani viongozi wa mataifa mengine huisoma nchi kupitia siasa, uchumi tunamalizia,” alisema Mwanaidi.

 

 

 

Imeandikwa na Shakila Mtambo, Prisca Pances (Dar), John Mhala, Veronica Mheta (Arusha), Nakajumo James,
Flora Mwakasala (Moshi) na Theddy Challe (Babati).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button