‘Michakato ya miradi ya maendeleo iharakishwe’

Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota.

MTWARA: WATENDAJI wa halmashauri ya mji Nanyamba mkoani Mtwara wametakiwa kuharakisha michakato ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wakati pindi wanapopata fursa ya miradi hiyo ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Mtimbwilimbwi wa kuendeleza madarasa ya kidato cha tano na sita katika halmashsuri hiyo, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota amesema watendaji hao waharakishe michakato hiyo kwa wakati ili fedha iliyopelekwa na serikali itumike ipasavyo.

“Tuharakishe michakato yote, upatikanaji wa zabuni, material yapatikane kwa wakati, ujenzi uende kwa wakati ili fedha ambayo imetafutwa ikaletwa hapa ilete matokeo chanya kwa wananchi wetu,”amesema Chikota.

Advertisement

Amehimiza kuzingatiwa kwa wazabuni wenye uwezo, wanaotoa huduma kwa wakati hususani kwenye upande wa manunuzi ili kuepuka changamoto ya kutokuwepo kwa vifaa kwenye eneo la mradi.

Soma:Sh bilioni 1 kujenga sekondari Dinyecha

Katika hatua nyingine Chikota ametembelea miradi ya maji Njengwa na Majengo uliotekelezwa na Wakala ya Usambazaji Maji Usafi wa Mazingira Mazingira Vijijini (RUWASA) uliogharimu Sh milioni 883.2/-

Akisoma taarifa ya mradi huo, Kaimu Meneja RUWASA Wilaya ya Mtwara Omari Kayanda amesema changamoto iliyopo kwenye miradi hiyo ikiwa ni pamoja na wananchi kutolinda miundombinu ya maji wakidai kuwa sio jukumu lao.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara Vijijini Nashir Pontiya ameendelea kusisitiza juu ya wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji na kulinda miundombinu yake ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu.

“Tutunze chanzo cha maji, kule bonding tusiende kuharibu mazingira ya chanzo, maeneo mengi maji yalipatikana ila baada ya muda yakaisha kwa sababu chanzo cha maji vimeharibiwa, maji hayana mbadala bora umeme utawasha kibatari na kuna maeneo mengi changamoto hii imetokea,” amesema Pontiya.

Mkazi wa kijiji cha mbambakofi kwenye halmashsuri hiyo, Bakari Nandumi ameiomba serikali kuwaletea walimu na vitendea kazi kwa wakati ili shule hiyo itakapokamilika ianze kutumiwa na wananchi hao.

Mwenge wa Uhuru ukiwa Halmashauri ya Mji Nanyamba mwezi uliopita ulikimbizwa kwenye miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya shs Bilioni 7.73.

Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Msingi Maranje, Shamba la Miti lenye hekari 10 katika Kijiji cha Chawi, Uwashwaji wa Umeme (REA) katika Kijiji cha Chawi, Uendelezaji wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mkomo, Ujenzi wa Barabara ya lami yenye urefu wa kilometa moja iliyopo mtaa wa Kilimanjaro, Kikundi cha vijana Pambamoto na ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Umoja kilichopo kata ya Milangominne.