Michezo ya majeshi kuanza leo
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla leo atafungua mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa baraza hilo, Brigedia Jenerali Said Hamis Said amesema michezo inatarajiwa kufikia mwisho Septemba 15 ambapo mgeni ramsi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Michezo ya majeshi inaundwa na kanda nane ambazo ni Ngome iliyopo chini ya JWTZ na kanda nyingine ni polisi , magereza , uhamiaji , zimamoto na uokoaji , Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kanda ya Idara Maalumu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
SOMA: Kombe la Mkuu wa Majeshi Julai 20
Michezo itakayochezwa ni soka, netiboli, basketi kwa wanaume na wanawake, volleyball riadha wanaume na wanawake zikiwemo za mbio za kilometa 21.
Mingine ni mpira wa mikono, mirusho ,vishale (Darts) na mchezo wa shabaha kwa kutumia silaha za moto ambayo itafanyika kwenye viwanja vya wazi isipokuwa wa shabaha ambao utatumika katika viwanja maalumu vilivyoandaliwa kutumia silaha hizo.