DAR ES SALAAM: JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni Dar es Salaam, limepanda miti 500, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji katika mkoa huo, Elisa Mugisha ameeleza hayo baada ya kukamilisha upandaji miti aina ya miembe, mitiki na midodoma.
“Tupo kwenye zoezi la upandaji wa miti ambalo awali tulijipangia kupanda miti isiyopungua 100 lakini tumeenda Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS), huko tumepata miti 500 ambayo tunaipanda kwenye viwanja vyetu viwili,” amesema.
Amesema miti hiyo wameipanda katika maeneo ya Luguruni Wilaya ya Ubungo na Mbweni Kinondoni.
“Tunashukuru wataalam wa misitu kutoka Ubungo na Kinondoni tumeshirikiana nao na kupata utaalam wa jinsi ya kupanda miti kwa sababu usipoangalia unaweza kupanda vibaya.
“Kilichobaki kwetu ni kutunza na kuhakikisha miti inakua na kufikia malengo tuliyojipangia. Tunaahidi itakuwa yote 500,” amesema.
Akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo, Mhifadhi David Nkya kutoka Wilaya ya Kinondoni na Ubungo mkoani Dar es Salaam, amesema wamefika eneo la Luguruni kwa ajili ya kushirikiana na Jeshi la Zimamoto kuwaelekeza namna ya kupanda miti ambayo wameitoa katika vitalu vya TFS.
“Tumewaonyesha jinsi ya kupanda kwa hiyo iliyobaki kwao ni suala la kuisimamia ili iweze kukua kama wanavyokusudia,” amesema.