Mikakati yawekwa kupaisha Soko la Kisutu

UONGOZI wa Soko la Kimataifa la Kisutu la mkoani Dar es Salaam unatarajia kuweka mabango makubwa kulitambulisha soko hilo kwa lengo la kuvutia zaidi wateja kwenda sokoni hapo.

Meneja wa soko hilo lililopo katika Kata ya Mchafukoge Wilaya ya Ilala, Happy Njovu alisema hayo alipozungumza na HabariLEO. “Tunategemea kuweka mabango makubwa ya kutambulisha soko letu,” alisema.

Njovu alisema pamoja na jitihada hizo, pia wanawarudisha sokoni wafanyabiashara wanaokwenda mtaani kufanya biashara zao.

Advertisement

Alisema Kisutu ni soko la kimataifa kwa sababu limekuwa likihudumia watu tofauti kutoka kwenye balozi na lipo mjini.

“Bidhaa zinazovutia kwenye soko letu ni mbogamboga na matunda kwa sababu ukija kwenye soko la Kisutu utakutana na mboga ambazo inawezekana huzifahamu na matunda adimu ambayo si rahisi kuyapata katika masoko mengine ya Dar es Salaam,” alisema.

Alisema kwa sasa soko hilo lina wafanyabiashara 1,060 na uwezo wake ni kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 1,500.

Katibu wa bidhaa ya matunda sokoni hapo, Mustapha Nyinga alisema soko hilo linauza matunda tofauti ambayo hayapatikani kwenye masoko mengine ya kawaida.

2 comments

Comments are closed.