Mikindani, Mtwara wapongezwa hati safi

MTWARA: MKUU wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amezipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa kupata hati safi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hayo yamejiri kwa nyakati tofauti wakati wa vikao maalumu vya mabaraza ya madiwani wa halmashauri hizo kuhusu kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akizungumza katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kuhusu kujadili hoja hizo za CAG, mkuu huyo wa mkoa ameipongeza manispaa kwa kutekeleza vizuri miradi ya maendeleo na usimamizi mzuri wa miradi hiyo.
Pia ametolea mfano mmoja wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye manispaa hiyo ikiwemo ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Tandika iliyogharimu Sh milioni 560 ambapo ujenzi wake umekamilika ndani ya miezi minne na wanafunzi kuanza masomo.
Mbali na hili amewataka watendaji kwenye manispaa hiyo kuongeza usimamizi wa mapato yao kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato huku akisisitiza maeneo yote yaliyojengwa miundombinu kewnye manispaa ambayo hayana hati kuhakikisha yanakuwa na hati miliki.
‘’Kila eneo ambalo lina muindombinu ya halmashauri kama hakuna hati miliki muhkikishe inakuwa na hati miliki kwani ni muhimu sana,”amesisitiza Sawala
Meya wa Manispaa hiyo, Shadida Ndile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye manispaa hiyo.
Pia amemuagiza mkurugenzi wa manispaa hiyo na timu yake kuhakikisha wanakusanya fedha kupitia nyanzo mbalimbali vya mapato na matumizi sahihi pia kuendelea kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao pale inapobidi.