Mikoa 14 yapata huduma za kibingwa bobezi

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amesema jumla watu 34,767 wamepata huduma za kibingwa na bobezi katika awamu ya pili ya huduma ya madaktari bingwa wa Samia ambapo mikoa 14 imefikiwa kwa awamu ya pili.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya huduma za kibingwa bobezi katika hospitali 184 za halmashauri amesema huduma hiyo ilianza Septemba 16 hadi Novemba 17,2024.

Amesema kuwa wagonjwa waliofanyiwa huduma za upasuaji kati ya hao ni 2,173 katika vituo 97 katika Mikoa hiyo.

Advertisement

Alitaja mikoa 14 ambayo tayari imefikiwa ni Lindi, Mtwara, Dodoma, Manyara, Singida, Mbeya, Rukwa, Songwe, Katavi, Tabora, Kigoma, Morogoro, Pwani na Dar es Saalam.

“Wakitoka hapa Dar es Salaam wanaenda Tanga,Arusha na Kilimanjaro na wakimaliza huko wataenda  Iringa, Njombe na Ruvuma hadi Novemba 17,2024 watakuwa wamemaliza hospitali za Halmashauri 184 nchi nzima,”amesema.

Amesema katika utoaji huduma madaktari bingwa saba hadi nane watatoa huduma katika kituo kimoja ambapo kitakuwa na madaktari bingwa wa wanawake, watoto na watoto wachanga na upasuaji.

“Kuna wa magonjwa ya ndani, ganzi na usingizi,magonjwa ya kinywa na meno, muuguzi bingwa na mabingwa wa mifupa ya ajali,kila hospitali itafanya kazi kwa siku sita watatekeleza kutoa huduma za kibingwa na bobezi,”amebainisha.

Mhagama amesema mambo makuu wanayofanya ni kutoa huduma za kibingwa na bobezi, kujenga uwezo wa madaktari wenzao watakaowakuta.

Mengine ni kuimarisha wodi za watoto wachanga na upasuaji kwani kuna maeneo vifaa vipo lakini havitumiki kwa upasuaji huku lingine ni ujuzi wa matumizi ya vifaa tiba.

“Huduma za kibingwa zitatolewa kwa bei nafuu kwa watakaoshindika tulisema wapelekwe kwenye Taasisi zetu hadi hospitali ya taifa , kuna wagonjwa wenye kufanyiwa upasuaji kwa Sh 100,000 wamefanyiwa kwa Sh 10,000 kwa gharama ya Sh milioni moja walitoa sh 100,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma ya afya Uzazi ya Mama na Mtoto  Dk Ahmed Mwakani akimwakilisha katibu mkuu afya amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwapatia vifaa tiba kwaajili ya program hiyo.

“Kuna watu wako vijijini wanakosa huduma na kutokana na kufika vijijini wameokoa maisha ya watu wengi ,tutatengeneza awamu nyingine kuja kutoa huduma.

Ameongeza “Ninawaomba wanachi wasiache wagonjwa ndani hasa vijijini tufuatilie kwanini jirani yangu hatoki kuna magonjwa yakitibiwa mapema madhara yanapungua kabisa.