HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 685.5 kwa vikundi 129 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022.
Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Dk Peter Nyanja alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za maendeleo katika kikao cha baraza la madiwani.
Kati ya vikundi hivyo, 98 ni vya wanawake, 16 vya vijana na 15 vya watu wenye ulemavu ambapo wanawake walikopeshwa Sh milioni 536, vijana Sh milioni 126 na watu wenye ulemavu Sh milioni 23.5.
Alibainisha kuwa usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa mikopo hiyo umewezesha Sh milioni 447.5 kurejeshwa. Vikundi vya wanawake vimerejesha Sh milioni 351.2, vijana Sh milioni 69.3 na watu wenye ulemavu Sh milioni 26.9.
Alisema kurejeshwa kwa mikopo hiyo kulitoa fursa kwa vikundi vingine kuwezeshwa na Sh milioni 341 zilizorejeshwa zilikopeshwa kwa vikundi vipya 70 ambavyo awali havikunufaika.
Dk Nyanja alieleza kuwa ili kuhakikisha mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani inanufaisha wajasiriamali wote, halmashauri imeweka utaratibu wa kuwapa fursa za kushiriki katika maonesho ya kibiashara ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao.
Alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, wajasiriamali 72 wamewezeshwa kushiriki maonesho ya kitaifa na kimataifa, yaliyoandaliwa na taasisi mbalimbali ikiwamo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Maonesho ya East Africa (Juakali) na Maonesho ya Sabasaba ya mkoani Dar es Salaam.
Pia vikundi 95 vyenye wanachama 2,322, wanawake wakiwa 2,197 na wanaume 125 vinavyojihusisha na utoaji wa huduma za kifedha vimesajiliwa na kutambuliwa na vinaendelea kutekeleza shughuli zao kama kawaida.
Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, jamii imenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia uwezeshwaji wa asilimia 10 za mapato ya ndani.
Alitaja baadhi ya mafanikio waliyopata kuwa ni kuundwa kwa vikundi vipya 240 huku 193 vikiwa vimekamilisha taratibu zote na kusajiliwa, kutoa kiasi kikubwa cha mikopo kwa vikundi vyote na kufanikiwa kukusanya Sh milioni 448 za mikopo hiyo sawa na asilimia 70.