SERIKALI imetenga takribani Sh milioni 776.83 kwa ajili ya upanuzi wa zahanati ya kijiji na kata ya Nkome katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kufikia hadhi ya kuwa kituo cha afya.
Upanuzi wa zahanati hiyo kuwa kituo cha afya unahusisha ujenzi wa majengo matatu ya huduma kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya huduma za afya kwa wakazi wa kata ya Nkome.
Mganga Mfawidhi halmashauri ya Wilaya ya Geita, Anthony Charles amesema hayo mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 walipofika kukagua na kuweka jiwe na msingi.
Amesema majengo hayo matatu ni jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), Jengo la Maabara na Jengo la Wodi ya Wazazi ambapo ujenzi umehusisha Pesa za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) 2021.
“Ujenzi huu unatekelezwa kwa awamu mbili, na kusimamiwa na wakandarasi wawili tofauti akiwemo Tujenge Pamoja Afrika kwa mkataba wa Sh milioni 540.69 kwa hatua ya msingi na kupiga lipu.
“Pia kampuni ya GIPCO Construction Limited kwa mkataba wa Sh milioni 236 .76 kwa hatua ya ukamilishaji na kufanya jumla ya mkataba kuwa Sh 776.83,” amesema Anthony.
Amesema ujenzi huo ulianza Julai 27, 2023 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 31, 2024 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 90 za ukamilishaji huku sh milioni 446.86 zimeshalipwa kwa wakandarasi.
Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku amesema upanuzi wa zahanati ya Nkome utasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto kwani zaidi ya watoto 600 wanazaliwa kwa mwezi katika kata hiyo.
Amesema upanuzi wa zahanati hiyo unaenda kufanya idadi ya vituo vya afya kufikia nane ndani ya halmashauri hiyo ambapo zimeondoa changamoto zilizokuwepo hapo awali.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Godfrey Mnzava amesema mradi huo ni utekelezaji wa dhamira ya serikali kuokoa maisha ya mama na mtoto na kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema mbali na mradi kutekelezwa kwa wakati lakini ni lazima Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifuatilie na kujua matumizi sahihi ya fedha za CSR katika mradi huo.