TUME ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imetenga jumla la Shilingi milioni 339 kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta zitakazosambazwa katika ofisi ya mrajis wa mkoa na wilaya na kuunganishwa kwenye mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa vyama vya ushirika nchini.
Mhasibu mkuu wa Tume hiyo Valency Karunde amesema hayo Disemba 7, 2022 kuwa fedha hiyo imetengwa kwenye bajeti ya m waka wa fedha 2022/2023 .
“ Katika kutekeleza mpango huu kwenye bajeti yetu tumetenga jumla la sh milioni 339 kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta kwa ajili ya kuzigawa kwa kila ofisi ya mkoa na wilaya ya mrajis wa Ushirika na mchakato huu umeanza na kompyuta 103 zimenunuliwa na kusambazwa” amesema Karunde
Karunde amesema hadi mwezi sita mwakani (2023) ofisi zote za ngazi za mikoa na wilaya zitakuwa zimepatiwa kompyuta ambazo zitainganishwa kwenye mfumo huo utawaondolea watendaji kutumia karatasi katika shughuli za kiofisi.
Amesema faida za matumizi ya mfumo wa kielektroniki kwa vyama vya ushirika ni hatua ya uboreshaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za serikali kwenye ushirika, kuwezesha upatikanaji wa masoko kwa wakulima, kuinua uchumi wa wanaushiriki na wa Taifa kwa jumla.
“ Matumizi ya mpango huo utasaidia kuongeza mnyororo wa thamani kwenye kilimo kwa sababu mfumo utaleta taarifa sahihi hususani upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi hivyo wakulima watakuza kipato chao” amesema Karunde