Miriam Odemba kujenga vyoo shule ya Mwendapole

.DAR ES SALAAM; MWANAMITINDO maarufu nchini Miriam Odemba kupitia Taasisi ya Miriam Odemba Foundation, amepanga kujenga na kuboresha miundombinu ya vyoo katika Shule ya Msingi Mwendapole iliyopo Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na HabariLEO mapema leo, Odemba ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo, amesema kuwa  hatua hiyo ni kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri, lakini pia kurudisha kwa jamii kama ilivyo utaratibu wao.

“Lakini pia tutasaidia serikali kupunguza idadi ya wanafunzi kutokwenda shule kwa kisingizio cha kutokuwa na miundombinu mizuri na kuwafanya watoto wapende shule na ufaulu uongezeke,” amesema Odemba.

Advertisement

Amesema ujenzi wa miundombinu ya vyoo katika shule hiyo itaanza rasmi mwezi ujao, ambapo licha ya jitihada hizo, wanacholenga zaidi ni kusaidia wanafunzi wa kike kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na kusimama na wadau wengine kupambana na ukatili huo.

Mpaka sasa taasisi hiyo imeshafanya miradi mingi ikiwemo kutoa elimu ya kijinsia na kujitambua iliyoambatana na ugawaji wa taulo za kike kwa mabinti hao takribani 700 katika Shule ya Msingi Kibamba Sekondari.