MISRI: Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri na Mfalme Abdullah II wa Jordan wamezungumza kwa njia ya simu, wakisisitiza msimamo wao wa kutaka kuujenga upya Ukanda wa Gaza pasipo kuwahamisha Wapalestina.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili walionyesha upinzani wao dhidi ya mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani, ambao unataka kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza na kuhamisha eneo hilo chini ya utawala wa Washington.
Mazungumzo haya yalifanyika baada ya Mfalme Abdullah kukutana na Rais Trump mjini Washington, ambapo alieleza wazi upinzani wake dhidi ya pendekezo la Marekani la kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu ya Misri, Rais al-Sisi na Mfalme Abdullah walisisitiza umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas, na kutaka kuachiwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina na mateka wa Israel.
Aidha, walieleza umuhimu wa kuendelea kupeleka misaada ya kibinadamu ndani ya Gaza. SOMA : Hamas haitaachilia mateka zaidi kama ilivyotarajiw
Mfalme Abdullah pia alizungumza kwa njia ya simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, wakijadili hali ya wasiwasi inayozidi kuonekana katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ambapo hali ya usalama na kibinadamu inaendelea kuwa tete.