WAZIRI wa Mambo ya Nje, Uhamiaji na Wamisri Waishio Nje mwa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Dk Badr Abdelatty amesema bandari na ushirikiano mzuri ni miongoni kwa mambo yanayovuta wawekezaji katika nchi waje kuwekeza nchini.
Dk Abdelatty amesema hayo Dar es Salaam akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Misri.
“Rais Samia alikuja Cairo mwaka 2021 na 2022, tukakutana tena Dubai 2023, na hivi karibuni nilihudhuria mkutano huko Rio de Janeiro na kukutana naye kwenye mkutano wa G20 na anapokutana na sisi si kwamba anakuja kutembea, bali analeta ajenda za kuleta maendeleo nchini pamoja na Afrika kwa ujumla hivyo tumevutiwa na ndio maana tupo hapa,” alisema Dk Abdelatty.
Alisema ushirikiano wa Tanzania na Misri ni wa kimkakati na akasema Tanzania ni mshirika muhimu katika biashara na uwekezaji.
“Kupitia bandari zilizopo nchini hivyo biashara kupitia njia za bahari itafanikiwa na maendeleo yataonekana wazi. Pia tunataka Misri iwe lango la Tanzania kuingia Afrika Kaskazini na Ulaya kupitia makubaliano ya kibiashara kama Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na Mkataba wa Mercosur unavyosema,” aliongeza.
Alisema Tanzania haitakiwi kuonekana kama soko pekee, bali ijikite kuwekeza kwenye viwanda ili kutoa ajira zaidi kwa vijana kwa kuwa kuna vijana wengi nchini Misri na Tanzania wenye kuhitaji ajira.
“Tusipoandaa na kutengeneza nafasi zaidi za ajira, kisiasa na kiuchumi tutakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira hivyo basi tuna wajibu wa kuwekeza katika uzalishaji, usalama wa chakula, kidijitali, mapinduzi ya viwanda na matumizi ya akili bandia,” alisema Dk Abdelatty.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amehimiza
wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania watumie fursa hiyo kuitangaza nchi na si kuiangusha.
“Serikali imetoa nafasi kwenu, itumieni fursa hii vizuri, tunawategemea na msituangushe, tumieni malighafi tulizonazo kuitangaza nchi,” alisema Balozi Kombo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Stanslaus Nyongo alisema serikali imelenga kuongeza ushirikiano na Misri kupitia sekta za nishati, utalii, huduma za afya, gesi na mafuta, kilimo, pamoja na viwanda.