Missenyi kuunganishwa maji ndani ya siku 7

WANANCHI walioomba kuunganishwa maji wilayani Misenyi watapatiwa huduma hiyo ndani ya siku saba.

Kauli hiyo imetolewa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2022,  Sahili Geraruma, wakati akizindua mradi wa maji wa Byamutemba Byeju, wilayani Missenyi.

Amesema ili wananchi wanufaike vizuri na maji, ni vema  waunganishe nyumbani kwao, ili kupunguza muda unaopotea kufuata maji.

“Sera ya maji mwaka 2002 ni kuwa walau wananchi wafate maji ndani ya mita 400, naweza kusema  hata hizo mita ni nyingi sana.

“Kama wananchi wanataka kuunga mkono juhudi za serikali wahakikishe wanaunganisha maji majumbani kwao, hayo maji wanayoungaunishiwa wakishalipiwa hawatazidi siku saba, hivyo wananchi lipieni huduma za kuunganisiwa maji,”alisema Geraruma.

Aliwataka wananchi kuhakikisha  wanalinda na kuitunza miradi ya maji, kwani serikali inatoa fedha nyingi kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati.

Meneja wa Mamlaka ya Maji (Ruwasa), Wilaya Missenyi Andrew Kilembe,  alisema kuwa mradi wa maji Byamtemba Byeju, umekamilika kwa gharama ya Sh Milioni 512.8 utawahudumiwa wananchi 11,983 sawa na kaya 2,393.

Mbunge wa Jimbo la Kenge,  Frolent Kyombo alisema wananchi wa wilaya hiyo kwa miaka 10 iliyopita, asilimia 97  walipoteza muda wa ziada kufuata maji na baadhi walishindwa kuendelea na shughuli nyingine .

Alisema hivi karibuni serikali imeendelea kuboresha miradi ya maji katika Wilaya ya Missenyi mpaka kata na vijiji, ambavyo havina historia ya kuwa na maji kabisa wanapata maji Safi na salama, kupitia miradi inayosimiwa na Ruwasa.

“Mimi Kama mwakilishi wa wananchi, lazima niwashukuru Ruwasa, wilaya yetu wananachi  karibia asilimia 60, walikuwa wanapata maji sehemu moja na mifugo yao, yaani binadamu na mifugo wote waligombania maji, lakini taratibu historia ya Missenyi isiyokuwa na maji inafutika na miradi inasimamiwa kwa weledi, “alisema Kyombo.

Habari Zifananazo

Back to top button