‘Mitaala mipya imezingatia wenye mahitaji maalumu’

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Elimu Tanzania (TET), imesema mitaala mipya ambayo imeanza kutekelezwa mwaka huu imezingatia watu wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na wenye ulemavu.

Akizugumza na HabariLEO leo Julai 6, 2024,  Mkuza mitaala kutoka TET Auguster Kayombo, amesema vitabu vinavyotumika kwenye mitaala hiyo mipya vimezingatia watu wenye uoni hafifu na wenye ulemavu wa aina tofauti.

Kayombo amesema lengo la mitaala hiyo ni kuwa na elimu yenye kujenga uelewa wa stadi mbalimbali za maisha na ndio maana hata wenye mahitaji maalum wamejumuishwa katika mitaala hiyo.

Advertisement

Alikuwa akizungumza katika viwanja vya Julius Nyerere (Sabasaba), yanapofanyika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam.

Amesema mitaala ya elimu nchini itasaidia kuzalisha wahitimu wenye ujuzi na maarifa katika fani wanazosomea.

Amesema mitaala kwa darasa la kwanza na la pili, masomo ni Kusoma, Kuandika, Kuonesha umahiri msingi katika Lugha ya Kiingereza, Hisabati, Kuthamini Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kutunza Afya na Mazingira.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/tet-yawasilisha-mabadiliko-ya-mitaala-mipya-ya-elimu/

Masomo kwa darasa la tatu hadi la sita ni Kiswahili, English, Kifaransa, Kichina, Kiarabu, Hisabati, Historia ya Tanzania na Maadili, Elimu ya Dini, Sanaa na Michezo, Sayansi na Jiografia na Mazingira.

Kwa elimu ya sekondari hatua ya chini, masomo ni Historia ya Tanzania na Maadili, Historia, Jiografia, English, Literature in English, Kiswahili, Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Michezo, Biolojia, Kemia, Fizikia, Kilimo, Hisabati, Sayansi ya Kompyuta na Utunzaji wa Taarifa za Fedha.

Pia masomo ya Elimu ya Biashara, Ushoni, Sanaa Sanifu, Muziki, Sanaa za Maonesho, Maarifa ya Nyumbani, Chakula na Lishe, Elimu ya Dini ya Kikristo, Elimu ya Dini ya Kiislamu, Fasihi ya Kiswahili.

Elimu ya sekondari hatua ya juu ni Historia, Jiografia, Elimu ya Dini ya Kikristo (Divinity), Elimu ya Dini ya Kiislamu, Kiswahili, English, Kiarabu, Kifaransa, Kichina, Fizikia, Kemia, Bailojia, Chakula na Kishe, Sayansi ya Kompyuta, Hisabati, Hisabati Tumizi (Basic Applied Mathematics).

Isome pia:https://habarileo.co.tz/mitaala-mipya-tec-tet-yawanoa-walimu/

Mengine ni Kilimo, Historia ya Tanzania na Maadili, Michezo, Sanaa Sanifu, Muziki, Sanaa za maonesho, Ushoni, Mawasiliano ya Kitaaluma, Elimu ya Biashara, Uhasibu, Uchumi, Fasihi ya Kiswahili, na Fasihi katika Kingereza.

Wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaoingia katika mkondo wa Elimu ya Amali na wa Elimu ya Jumla, watasoma kwa pamoja masomo matatu ya Elimu ya Michezo pamoja na masomo ya jumla.

Kidato cha pili, wanafunzi katika mkondo wa Elimu ya Amali watachagua michezo miwili na fani ambazo watazisoma na kubobea hadi kidato cha nne.