Mitungi ya gesi 500 wakabidhiwa wanawake Mufindi

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini Exaud Kigahe, amekabidhi mitungi ya gesi 500 kwa wanawake wa jimbo hilo yenye thamani ya Sh milioni 50 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema amejipanga vizuri kumuunga mkono Rais Dk Samia katika kutunza mazingira na kuondokana na uharibifu kwa kuendelea kuwawezesha wananchi na kuwahamasisha kutumia nishati safi kwa wanawake wa jimbo hilo.

Akizungumza jimboni humo, wakati wa kongamano la kukabidhi majiko hayo leo Kigahe amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kununua mitungi hiyo ya wananchi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa kuhamasisha nafasi hiyo.

“Tunamshukuru sana Rais Samia, kwa upendo wake huu mkubwa, kwani aliona changamoto iliyopo ya mabadiliko ya tabia ya nchi, inayotokana na ukataji kuni, mkaa na maendeleo ya viwanda, hivyo kuwasaidia wananchi kuepukana na nishati haribifu”. amesema.

Mbunge Kigahe amesema, dhamira ya Rais Samia kufanya hivyo ni kufahamu vyema changamoto ya kina mama kutafuta kuni na kuharibu mazingira hali inayoathiri uzalishaji wa chakula.

Amesema kutokana na matumizi ya kuni na mikaa baadhi ya maeneo nchini, yamekuwa na hali ya jangwa hivyo ndio maana na wao wanatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Dk.Samia ya kufikisha nishati safi kwa wananchi.

Amesema majiko hayo yanawasaidia kuzuia uharibifu na kutunza mazingira. Pia nishati hiyo inaokoa muda na kuwasaidia kufanya shughuli za uzalishaji.

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendegu, amempongeza mbunge huyo, kuendelea kutekeleza ajenda ya Rais Samia, ya kutunza mazingira kwa kuhamasisha nishati safi ya gesi na mkaa mbadala, kuachana matumizi ya kuni.

Amesema athari za mabadiliko ya tabia ya nchi yanayotokana na uhabifu wa mazingira ya ukataji kuni za kupikia na kutengeneza mkaa.

Amesema matumizi ya nishati safi ya gesi inasaidia kuokoa muda wa kufanya shughuli za uzalishaji na kuwaweka katika hali ya usafi na kuimarika ndoa. Amesema wataendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika Mkoa huo uwe salama zaidi kwa kuwa na asili yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx gas, Benoit Araman amesema wanamuunga mkono Rais Samia kufikisha nishati safi kwa wananchi. Amesema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza nchini kuhakikisha wanaongeza matumizi ya nishati safi.

Habari Zifananazo

Back to top button