Mitungi ya mil 100 yagaiwa wakazi Dar

KAMPUNI ya Total Energys imetoa mitungi ya gesi 2,000 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100 ili kuwakinga wanawake dhidi ya matumizi ya nishati chafu inayoweza kusababisha madhara kiafya.
Mitungi 1,000 itapelekwa Arusha iliyobaki itagaiwa mkoani hapa.

Mitungi hiyo imegaiwa leo Machi 4,2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji,Profesa Kitila Mkumbo wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kanda ya Dar es Salaam na Pwani.
Mkurungenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Mamadou Ngome amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza maeneo yote nchini kutumia nishati safi ya kupikia na kuacha matumizi ya nishati chafu ilikulinda afya.

“Nishati safi kama matumizi ya umeme, gesi na joto la ardhi ni nyenzo kuu kwa taifa letu kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi hivyo niwaase wananchi kuacha matumizi ya nishati chafuzi kama mkaa na kuni ambazo zinaharibu mazingira na kusababisha magonjwa ya upumuaji, vifo na athari nyingine za kijamii,”amesema Ngome.
Amesema: ”Changamoto nyingine ni katika familia kwani ndoa nyingi huvunjika, hivyo ndugu zangu natoa wito kwa wananchi wote suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira ni jukumu la kila mtu hasa kwa kutumia nishati safi,leo tumegawa mitungi hii isiwe mwisho wa matumizi yake pale inapoisha gesi bali uwe mwendelezo”.

Kwa upande wake Profesa Kitila Mkumbo aliwataka wanawake hao kuhamasasisha wengine katika matumizi ya nishati safi ilikuweza kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na taifa kwa ujumla.
“Fursa zipo nyingi nchini jitahidi kwa hali na mali mzitumie acheni kuwa wanyonge,pambana ili kukuza uchumi wako na taifa zima,”Profesa Mkumbo.


