Mizimu yatumika kukatisha masomo wasichana, kuwaozesha Kwimba

MWAMKO mdogo wa elimu kwa wazazi waishio wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, umekuwa kikwazo kwa watoto wa kike kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari, badala yake wanalazimishwa kuolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
Vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto huanza kutekelezwa pale mtoto anapokaribia kuhitimu elimu ya msingi au akiwa sekondari.
Vitendo hivyo ni kinyume cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, ambayo inatamka kwamba mtoto ni yule mwenye umri wa chini ya miaka 18 na kwamba miongoni mwa haki anazopaswa kupatiwa ni elimu.
Kadhalika, Sheria ya Elimu namba 5 ya mwaka 1979 inatamka kwamba ni kosa kwa mtu yeyote kukataa kumpa fursa ya elimu rasmi mtoto kwa misingi ya jinsia, imani, itikadi za kisiasa au hali ya kiuchumi na kijamii.
Hivyo, wazazi wanaotekeleza unyama huo wanakwenda kinyume cha matakwa ya sheria na sera, pia wanachangia kuwa na jamii isiyokuwa na elimu, wasichana kushindwa kujitegemea kiuchumi, unyanyasaji wa kijinsia na vifo vya uzazi.
Sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023 yenyewe imeweka masharti ya lazima kwa mtoto kusoma miaka 10 kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, lengo ni kumuwezesha kuongeza ujuzi na kuchangia katika uchumi.
Akizungumza kuhusu mbinu wanazotumia wazazi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bupamwa iliyopo Kwimba mkoani Mwanza, Herman Shingisha anasema wazazi wa jamii ya Wasukuma hutumia masamva (mizimu au roho za mababu walioishi zamani) kuwakatisha watoto wao kuendelea na masomo.
Mwalimu Shingisha anaeleza kwamba sababu wanazozitoa wazazi hao kuhusu mizimu ni kuwa inamfanya mtoto kushindwa kuendelea na shule, kusababisha kutokuona kinachoandikwa ubaoni na kutoelewa kinachofundishwa darasani.
Takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2021, matukio ya ukatili kwa watoto yaliyoripotiwa ni 11,499 na mikoa wa Mwanza ulishika nafasi ya nne kwa kuwa na matukio 500 ya ukatili. Hata hivyo, makosa ya kukatisha masomo yaliyoripotiwa mwaka huo yalikuwa 790.
Pia, takwimu hizo zilibainisha Mkoa wa Mwanza uliongoza kwa matukio ya mimba za utotoni kwa shule za msingi (98) na sekondari (491).
Anasema licha ya kutokuwa na takwimu sahihi kuhusu wanafunzi wake wa kike wanaoacha shule na kuolewa, kiashiria cha awali cha uwepo wa ndoa za utotoni kwa wasichana hao ni utoro shuleni.
Mwalimu Shingisha anabainisha: “Tunapobaini utoro wa wanafunzi wa wiki moja au mbili, tunatoa taarifa kwa mtendaji kwa ajili ya ufuatiliaji, lakini hatupati mrejesho kama wanafunzi wetu wako wapi na mzazi anapohojiwa anasema mtoto wake ana masamva au mizimu.”
Anaeleza bila wao kujua, katika kipindi hicho wazazi wanakuwa kwenye majadiliano ya ndoa na baada ya kuwaozesha mbali na maeneo wanayoishi, wazazi wanakimbia makazi yao na kuhamia sehemu nyingine kukwepa mkono wa sheria.
Takwimu za Msingi za Elimu zinazotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (BEST) za mwaka 2021 zilionesha idadi ya wasichana walioacha shule za sekondari kwa sababu ya utoro wilayani Kwimba mkoani Mwanza walikuwa 909, huku kidato cha pili wakiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wasichana wapatao 340.
Katika takwimu hizo, pia ilibainishwa kuwa mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliacha shule kwa sababu ya ndoa.
Mwaka 2022, kulikuwa na ongezeko la wanafunzi 227 walioacha shule kwa sababu ya utoro hivyo idadi yao kuwa 1,136 ikilinganishwa na walioripotiwa 2021. Hata hivyo, mwaka 2023, walioacha shule kwa sababu hiyo hiyo walikuwa 1,287 kwa shule za sekondari.
Takwimu hizo zinaifanya wilaya ya Kwimba kuongoza kimkoa kati ya wilaya nane, kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha shule jambo linalohatarisha ustawi wa maendeleo ya wananchi wake.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Kijiji cha Chasalawi, George Pamba, anasema kwa wastani anapokea kesi tano za utoro kwa mwaka hususan wakati wa kufungua shule (Januari na Juni) na hatua wanazochukua ni kufuatilia kwa wazazi kujua tatizo linalochangia mtoto kutofika shuleni.
Anasema moja ya kesi aliyopokea mwaka jana ni ya mwanafunzi wa sekondari mwenye umri wa miaka 15 ambaye aliacha kwenda shule takribani wiki mbili na walipofuatilia walibaini wazazi wake walipokea mahari ili aolewe.
“Kwa kushirikiana na kamati ya kijiji, tulifuatilia na kuzuia ndoa hiyo na ng’ombe zilirudishwa na sasa mtoto anaendelea na masomo,” anasema.
Naye Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kwimba, Mwalimu Emmanuel Katemi, anasema mwaka 2024 walifanikiwa kuzuia ndoa tatu za wanafunzi. Mojawapo ilikuwa ya mwanafunzi ambaye alichaguliwa kwenda sekondari na mwengine alikuwa amechaguliwa kwenda kidato cha tano.
Mwalimu Katemi anasema walipofuatiliwa kesi hizo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walibaini wazazi waliwakataza watoto hao kusoma na kupokea mahari ya ng’ombe ambazo walizichukua na kupeleka magereza kisha watoto hao wakarudishwa shuleni.
“Nikiri kwamba ndoa za utotoni hapa kwetu zipo na hali ya watoto kuacha shule inatokokana na mwamko duni wa wazazi na umasikini, wanadhani ng’ombe wanazopata zitawasaidia kukabiliana na umasikini,” anasisitiza.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Chasalawi, Mugalula Kasululu, anasisitiza kuwa ndoa za utotoni huanzia kwa wazazi kuwakataza watoto wao kujaza majibu sahihi kwenye mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ili wasifaulu.
“Tunapata watoto wengi wazuri, wanafanya vizuri katika mitihani yote ya ndani na ya mkoa, lakini mzazi anamshawishi ajaze madudu na kumtolea mfano hasi kuhusu watoto wenzao waliosoma na kukosa ajira,” anasema Mwalimu Kasululu.
Anasema hali hiyo huwafanya watoto kutoendelea na masomo na baada ya kukaa nje ya mfumo wa elimu, huamua kuwaozesha.
Mwanafunzi Anitha Julius (si jina halisi), anasema ameshuhudia wanafunzi wengi wa kike wanaoripoti kwa wiki moja, mbili au mwezi mmoja wanapoingia kidato cha kwanza kisha wanaacha na kwenda kuolewa.
Anasema wengine huendelea na masomo hadi kidato cha pili kisha wanajifelisha katika mitihani yao kwa madai kwamba wazazi wao wanawataka waolewe hivyo wakifaulu hawatasomeshwa.
“Wapo wanafunzi wengi wanaolewa, kwa mfano sisi tulianza sekondari zaidi ya 200 lakini tulifika kidato cha nne tulikuwa 96 lakini wenzetu watatu waliolewa mwezi wa tisa tulipokuwa tunakaribia kufanya mtihani wa kidato cha nne,’’ anaeleza.
Anafafanua ‘’ Wanafunzi wengine wanapewa maelekezo na wazazi wao waripoti kisha waache shule, baadhi ya wazazi wanadai hawana fedha za kuwasomesha wakitaka kuendelea watajua wenyewe, inakatisha tamaa.’’
Umbali wa shule unavyochangia mdondoko wanafunzi
Sababu nyingine inayotajwa kuchangia wazazi kuwaoza mabinti wakiwa chini ya umri wa miaka 18 hususan wanafunzi, ni umbali kutoka nyumbani kwenda shule, wakilenga kuepusha aibu nyumbani mwao, wakiamini kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kupata mimba.
Shule ya sekondari Bupamwa ilikuwa inapokea wanafunzi kutoka vijiji sita vya Itegamatu kilichopo umbali wa Kilometa 40, Kijiji cha Dodoma (22), Kijiji cha Kiliwi (15), Mwambisu (16), Chasalawi (12) na Mhalo (10).
Akielezea kuhusu changamoto hiyo, Mwalimu Shingisha anaeleza umbali huo unachangia idadi ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza kutolingana na wale wanaomaliza kidato cha nne.
“Mwaka 2021 wanafunzi walioanza kidato cha kwanza walikuwa 168 na waliomaliza ni 65, mwaka 2022 walioanza ni 153 na waliohitimu ni 61, mwaka 2023 walioanza ni 183 na waliohitimu walikuwa 93, kadhalika mwaka 2024 walioanza walikuwa 202 na waliohitimu ni 96,’’ anafafanua.
Anasema katika kipindi cha miaka minne kutoka 2021 hadi 2024, jumla ya wanafunzi 391 waliacha shule kati yao 182 walikuwa wasichana hali inayotishia ustawi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa kata hiyo na wilaya kwa ujumla.
Anatoa mfano ‘’ Wasichana walioacha shule mwaka 2021 walikuwa 52, mwaka 2022 walikuwa 40, mwaka 2023 walikuwa 40 na 2024 walioacha walikuwa 50.’’
Takwimu hizi zinaonyesha kwamba wanaomaliza shule ni wachache kuliko walioishia njiani, ambao ni wastani wa asilimia 60, hali hii inakinzana na juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa ya elimu sawa na watoto wa kiume.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwamashimba, Ngole Mwanzalima anasema mwaka 2021, takribani wanafunzi 80 hawakujulikana walipo ndani ya mwaka mmoja hivyo alitakiwa kujieleza.
“Ukweli ni kwamba ndoa za utotoni miongoni mwa wanafunzi wetu zipo, isipokuwa hatupati mrejesho kutoka kwa watendaji; jamii ya Wasukuma wapo zaidi kifugaji na sio kisomi,” anasema Mwalimu Ngole.
Wadau walonga
Ofisa Mradi wa Shirika lisilo la kiserikali la Amani Girls, Bahati Mang’olo, anasema wako katika maandalizi ya kuanza mradi wa kupinga ukatili dhidi ya watoto kupitia uboreshaji mabaraza ya watoto utakaofanyika katika shule nane za msingi ambazo ziko katika kata ya Bupamwa na Kikubiji.
Lengo ni kuyajengea uwezo mabaraza hayo katika kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwamo ndoa za utotoni.
“Elimu tutaitoa kwa watoto kupitia mabaraza yao na sababu ya kuja na mradi huu tulifanya utafiti katika eneo hili tukabaini watoto wengi wanaolewa baada ya kumaliza darasa la saba na wanapojiandaa kwenda kidato cha kwanza,” anasema.
Pia, watoto wanaofaulu hawaendelezwi na wapo wanaoacha shule na kuolewa.
“Hakuna mtu anayezuia ndoa za watoto ambao wako nje ya mfumo wa elimu na badala yake kelele zimekuwa kwa wale wanaosoma tu,” anaeleza Mang’olo.
Anasisitiza wanapaswa kupinga ndoa zozote zinazohusu watoto chini ya umri wa miaka 18 kwa sababu zina athari kijamii, kiuchumi na kiafya.
Hatua zinazochukuliwa
Pamba ambaye ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Chasalawi anasema wanatumia jeshi la jadi la Sungusungu kama njia ya kukabiliana na utoro na kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao shule.
Pia anasema, wanatoza faini ya mifuko mitatu ya saruji wazazi ambao hawapeleki watoto wao shule, ili kuhakikisha wanatekeleza sheria zilizowekwa nchini.
Mwalimu Shingisha anasema wameamua kuweka kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne kuepuka mazingira hatarishi ya nyumbani kwao na kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu.
“Kambi hii imetusaidia kuwa na matokeo mazuri kiwilaya na mako, lakini hata kwa matokeo ya kidato cha pili mwaka huu ni mwanafunzi mmoja tu wa kike alijifelisha,” anafafanua.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija, anasema jamii ya Kisukuma haijaweka kipaumbele kwenye elimu ya mtoto wa kike, ndio maana ndoa za utotoni bado zipo na kwamba wameanza uhamasishaji wa watoto wa kike kusoma kwa kuwapa mifano hai ya viongozi wanawake ambao wamefanikiwa kupitia kusoma.
“Nikiri Usukumani hili suala la ndoa za utotoni ni kubwa. Hatua tunazochukuwa ni kutaifisha mahari (ng’ombe) zinazotolewa na kuwa mali ya serikali na mtoto anarudishwa shuleni,’’ anasema Ludigija.
Anasema msisitizo umewekwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi kwa wakuu wa shule kwa kumpatia mtoto namba maalum wakati anaporipoti, na watakapobaini ameacha shule na kuolewa, viongozi hao watachukuliwa hatua kwa kuhusika na vitendo hivyo.
Katika kukabiliana na umbali, Ludigija anasema wameanza kuainisha maeneo ambayo yanahitaji kuwa na shule na kwamba katika kata ya Bupamwa imeongezwa shule ya sekondari Mihayocheyo kupunguza umbali.
“Umbali kwa shule ya msingi unapaswa angalau uwe kilometa tano na sekondari hazitakiwi kuzidi kilometa saba. Nimeelekeza maofisa elimu kata kuhakikisha watoto hawapangiwi shule za mbali kwa sababu tu ya kata badala yake wanafunzi ambao si wa kata husika, lakini wako karibu wapangiwe huko kuepusha umbali usio na lazima,’’