Mjadala wa bandari wamuibua Sheikh Khalifa

Ataka watu kutumia maneno ya staha

MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukary, Sheikh Khalifa Khamis, ameshauri mjadala kuhusu uendelezaji wa bandari ujikite kwa kujenga hoja na kutoa mapendekezo kwa nia ya kupata suluhisho lenye manufaa kwa Watanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijadili suala hilo kwa kutumia maneno yasiyo na staha kwa nia ya kueneza chuki miongoni mwa watanzania.

Amesema, Rais Samia ana lengo la kuboresha ufanisi wa shughuli za bandari uwe na tija ili Serikali ipate fedha zaidi kwa manufaa ya watanzania wote.

“Kila Mtanzania ana haki ya kujadili ama kutoa maoni yake juu ya taasisi yoyote ya umma, lakini jambo hili lazima lifanyike kwa kujenga hoja, kutoa mapendekezo kwa nia ya kupata suluhisho lenye manufaa kwa watanzania.

“Wanaopinga wawe na hoja za msingi, watanzania wajiepushe na mijadala ya ubaguzi na udini kwa sababu sisi sote ni wamoja,” amesema Sheikh Khamis.

Amesema, pia baadhi ya vitengo vya bandari vimekuwa vikiendeshwa kwa ubia baina ya Mamlaka ya Bandari na kampuni zisizo za Serikali hivyo kinachotaka kufanywa sasa si jambo jipya.

Mwenyekiti huyo ameshauri wananchi waeleweshwe kuhusu manufaa ya uwekezaji huo na uwezo wa kampuni husika na maoni yao yasikilizwe.

Juni 10, 2023 Bunge lilipitisha azimio kuhusu makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Dubai Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button