Mji mkongwe kuendelea kuhifadhiwa

ZANZIBAR : RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wadau  kuungamkono juhudi za kuutunza, kuuhifadhi na kuuendeleza Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na umuhimu wake kwa Uchumi wa nchi.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na ujumbe kutoka Taasisi ya “International National Trust Organization” ya Uingereza iliyomueleza mafanikio waliyoyapata katika kulifanyia ukarabati jengo la “Custom House” liliopo Forodhani maarufu jengo la Mizingani.

Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema Mji Mkongwe mbali ya kuwa ni eneo la Urithi wa dunia pia ni eneo muhimu katika kukuza Uchumi wa Zanzibar kupitia Sekta ya Utalii.

Advertisement

Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarijika na juhudi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe (JUHIMKO) kwa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Mizingani.

Akizungumzia changamoto za mabadiliko ya Tabianchi, ikiwemo kuongezeka na kina cha bahari, Meneja miradi wa Taasisi ya “International National Trust Organization”, David Antony Simpson amesema ni miongoni mwa changamoto inayoikabili miji mingi ya urithi duniani iliyoko pembezoni mwa bahari kama ilivyo kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar, na kuahidi taasisi yake kuendeleza ushirikiano na Zanzibar kuhakikisha Mji Mkongwe kubaki kwenye ramani ya dunia.

SOMA : Rais Mwinyi asema mji Mkongwe utabaki kama ulivyo

Vilevile ameeleza kuwa taasisi hiyo ina uzoefu kwa nchi 102 duniani walizozifanyia ukarabati wa miji mikongwe.