Rais Mwinyi asema mji Mkongwe utabaki kama ulivyo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha Mji Mkongwe unabaki kama ulivyokuwa miaka 200 iliyopita na si kuubadilisha.

Dk Mwinyi amesema hayo katika hafla fupi ya ufunguzi wa Jengo jipya la Hoteli ya Tembo, iliyofanyika Ukumbi wa Tembo House Hoteli ,Shangani leo Machi 22, 2023 Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema wapo wanaojaribu kupotosha kuwa serikali ina lengo la kuubadilisha Mji Mkongwe kwa kuugawa na kubinafsisha na akaeleza lengo ni kuwapa watu wenye uwezo kuyajenga majengo hayo , kuyatunza ili yaweze kudumu miaka 200 ijayo akitolea mfano Jengo la sasa la Tembo Hoteli lilikuwa Ubalozi wa Marekani mwaka 1831 na Jengo lililozinduliwa leo kwa marekebisho ilikuwa ni Skuli mwaka 1944.

Aidha, Rais Dk Mwinyi amewakaribisha wawekezaji waje kushirikiana na Serikali kurudisha hadhi ya Mji Mkongwe na kuujenga huku akitoa miezi mitatu kwa waliopewa Majengo mbalimbali kwa ajili ya kuyarekebisha na kuyaendeleza wakishindwa Serikali itayachukua .Pia ameeleza Serikali imeamua kutenga fedha kuhakikisha inaleta mfumo bora wa maji, mfumo wa kisasa wa umeme , huduma ya Internet, ujenzi wa barabara katika Mji Mkongwe ili kuwa kivutio kwa utalii.

Amemshukuru Mfalme wa Oman Sultan Haitham Bin Tariq M Said na Serikali yake kwa msaada wa Dola za Kimarekani Milioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Beit-al-Ajaib na kulirudisha katika hadhi yake na mkandarasi ameshapatikana na ujenzi utaanza hivi karibuni.

Habari Zifananazo

Back to top button