Mkakati kuhakikisha usalama, ubora vyakula vya mifugo

SERIKALI imekutana na Vyama vya Ndege Wafugwao pamoja na Chama cha Wazalisha wa Vyakula vya Mifugo (TAFMA), ili kuhakikisha usalama na ubora wa vyakula vya mifugo nchini.

Hatua hii imekuja muda mfupi baada ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kukamilisha ukaguzi wa baadhi ya viwanda vya vyakula, na kukuta baadhi yake vina uvunjifu mkubwa wa sheria.

“Tumeanza kufanya kazi kwa karibu na vyama vya mifugo nchini na mkutano wa leo, tumeanza na Chama cha Wazalishaji wa Vyakula vya Mifugo nchini (TAFMA) pamoja na vyama vya ndege wa wafugwao,” amesema Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari, Dk Dk Stella Bitanyi.

“Vikao hivi vinalenga kusimamia usalama na ubora wa mifugo, maana wafugaji wadogo nchini wanategemea wazalishaji wa vyakula vya mifugo kuzalisha vyakula bora ili kuongeza tija kwa wafugaji na wapate matokeo mazuri ya mifugo yao.” Amesema Dk Stella Bitanyi.

Dk Bitanyi amesema serikali itahakikisha inasimamia suala la ubora na wakala hiyo itakuwa na mikutano ya mara kwa mara, kutoa elimu, kutembelea maeneo yanayotengenezwa vyakula vya mifugo na kusimamia ubora.

Wadau waliohudhuria kikao hicho wameomba kuwepo kwa vikao vya mara kwa mara ili kuwakumbusha wazalishaji wa vyakula vya mifugo kuzalisha vyakula bora.

Wamekiri kunufaika na elimu inayotolewa na TVLA pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyakula vya mifugo nchini ili kuhakikisha wafugaji wanapata vyakula bora na hatimaye kufikia malengo ya ufugaji wao.

Habari Zifananazo

Back to top button