Mkakati mpya wa Mantra kuinua uchumi, kugusa jamii Namtumbo
KAMPUNI ya uchimbaji wa madini ya urani imeahidi kusaidia maendeleo ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kupitia sera yake ya uwajibikaji wa jamii (CSR).
Ahadi ya Mantra Tanzania imetolewa katika kongamano la biashara la Namtumbo Kihenge lililofanyika Septemba 21 hadi 22, mwaka huu.
Katika kongamano hilo, mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Ng’waniduhu, alisema tukio hilo limeleta matumaini na ni muhimu kwa wilaya hiyo kwani limetoa fursa ya majadiliano, makubaliano na kubadilishana mawazo ya kibunifu ambayo yanaweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo endelevu katika eneo hilo.
Mantra, kama mdau muhimu wilayani humo, ilishiriki katika kongamano hilo na kuweka bayana namna jamii inaweza kunufaika kupitia mradi wake.
Akitoa shukrani zake kwa Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo kwa kuandaa jukwaa la Namtumbo Kihenge 2023, meneja wa uendelevu wa Mantra Tanzania alieleza faida za mradi huo zikiwemo ajira na biashara kama sehemu ya matokeo ya maendeleo yatokanayo na shughuli za uchimbaji.
“Mradi wa Mantra si uchimbaji wa urani pekee,” Majani aliwaelezea washiriki. “Bali ni utengenezaji wa fursa zitakazoweza kuinufaisha jamii yote. Kutoka ajira za moja kwa moja kwenye mradi hadi ajira zisizo za moja kwa moja zinazozalishwa na mahitaji ya bidhaa na huduma. Mradi huu ni kichocheo cha ukuaji wa kiuchumi.”
Katika manufaa ya kiuchumi, Majani aliwaeleza washiriki kuhusu mkakati wa uwajibikaji wa kampuni ya Mantra kwa jamii wa miaka mitano (2023-2028) ambao umejikita katika katika maneno ya afya, elimu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii.
“Mkakati wetu wa uwajibikaji kwa jamii si tu kurudisha kwa jamii,” alisema Majani na kuongeza: “Ni uwezeshaji kwa jamii iliweze kuchukua hatamu ya maendeleo yake. Tunataka kutengeneza mfumo endelevu wa maendeleo ambao utaendelea kuinufaisha jamii hata baada ya mradi huu kuisha.”
Uwajibikaji wa Mantra kwa jamii umeenda zaidi ya yaliyoainishwa katika mpango wake wa CSR. Kampuni hii ni miongoni kwa wadhamini wakuu wa jukwaa la Namtumbo Kihenge la mwaka huu na imeahidi kuendelea kusaidia majukwaa kama hayo pamoja na ptrogramu ambazo zitakuwa na matokeo chanya ya kiuchumi katika ngazi ya wilaya, mkoa pamoja na nchi.
“Tunaamini katika nguvu ya ushirikiano na ushirikishwaji wa jamii,” alisema Majani. “Kwa kudhamini majukwaa kama hili la Namtumbo Kihenge, tunahimiza utamaduni wa majadiliano na ubunifu ambao utaharakisha maendeleo ya wilaya.
”
Huku Mantra Tanzania ikiendeleza mradi wake wa urani, kampuni hiyo bado imeendelea kutekeleza ahadi zake za kuisaidia wilaya ya Namtumbo kupitia sera yake ya uwajibikaji (CSR) na kusaidia shuguli za kijamii.
Kupitia jukwaa hilo, Mantra Tanzania ilipata cheti cha shukrani kutoka ofisi ya Halmashauri ya Namtumbo ambayo ilitambua mchango mkubwa wa kampuni hiyo katika tukio hilo.
Kampuni hiyo ina rekodi ya muda mrefu ya kushiriki katika jamii na mchango wake katika maandalizi ya jukwaa hiyo ni muendelezo wa jitihada zake za kuinua uchumi wa mkoa. Kutambuliwa kwake katika tukio hilo ni ushahidi wa wazi wa namna inavyojitoa pamoja na juhudi katika kazi.
Akizungumza katika jukwaa la Kihenge, Mbunge wa jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa aliwataka wananchi kutumia kongamano hilo la kibiashara kuvutia wawekezaji wakubwa katika sekta za kilimo na madini kwani wilaya hiyo ina fursa kubwa ya kuchangia uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.
Mbunge huyo aliomba mamlaka za serikali kuunga mkono mradi wa uchimbaji urani wa Mantra Tanzania.
Mwanasiasa huyo anaamini kuwa endapo Serikali itaongeza jitihada, mradi huo unaweza kufanya kazi kwa kipindi kisichopungua miaka 15 na kuchangia hadi asilimia 20 ya uzalishaji wa urani barani Afrika, sawa na asilimia 4 ya uzalishaji wa madini hayo kidunia.
Hivi karibuni, Mantra iliandaa ziara ya madini kwa washiriki 150 kutoka jukwaa la biashara la Namtumbo, shughuli ambayo iliongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya shughuli za mgodi wa urani, usalama unaochukuliwa na Mantra wakati wa uchimbaji.
Zoezi hili lilifanyika katika eneo mgodi wa urani unaoendeshwa na Mantra lililopo ndani ya Mbuga ya Nyerere, takribani kilomita 54 kutoka makazi ya watu na kilomita 140 kutoka Namtumbo mjini.