Mkandarasi apewa miezi 4 shamba la mbegu Msimba likamilike

NAIBU Waziri wa Kilimo,  Anthony Mavunde,  amemtaka mkandarasi anayejenga miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Msimba kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati ifikapo mwezi Julai 2023 ili uzalishaji wa mbegu uanze kufanyika kwa kipindi chote cha mwaka.
Mavunde, ameyasema hayo  alipofanya ziara Msimba wilayani Kilosa,Morogoro ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
” Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa fedha za kujenga mradi huu, na ametusisitiza tusimamie matumizi ya fedha hizo kwenye miradi ili ziweze kuleta matokeo tarajiwa.”Amesema na kuongeza
“Hivyo, ujio wangu leo hapa ni kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huu ambao unahusisha uchimbaji wa visima vinne, fensi ya shamba pamoja na uchimbaji wa bwana lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 45 kwa ajili ya umwagiliaji.
Ninamtaka Mkandarasi ahakikishe anaishi ndani ya muda wa mkataba na kukabidhi mradi huu mapema mwezi Julai,2023 au kabla ya hapo.
Amesema, serikali ya awamu ya sita imeweka mkazo mkubwa kwenye kilimo, na ndiyo maana hata bajeti ya ASA imeongezeka kutoka takribani sh. bilioni 10 hadi sh bilioni 43, fedha ambazo zinawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi hii ikiwemo suala la uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yote ya mbegu ya Wakala.
Awali, akieleza juu ya Taasisi yake­, Afisa Mtendaji Mkuu wa ASA, Dkt. Sophia Killenga-Kashenge aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika uzalishaji wa mbegu bora na kubainisha kuwa kupitia uwezeshaji huo wamepanga kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yote 15 ya ASA ili kufanikisha kuzalisha mbegu bora hadi wakati wa kiangazi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa,  Shaka Hamdu Shaka alishukuru kwa ujio wa mradi huo wilayani Kilosa na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na ASA katika usimamizi na kutatua changamoto zote ili mradi uweze kumalizika haraka na kuanza kuwanufaisha wakulima wa Kilosa na Taifa kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Back to top button