Mkataba maboresho usafiri wa anga wasainiwa

DAR ES SALAAM; Tanzania na Oman zimesaini maboresho ya mkataba wa Usafiri wa Anga (BASA), ambapo Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameiwakilisha Tanzania kwenye utiaji saini huo na Oman imewakilishwa na Rais wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga wa nchi hiyo, Mhandisi Ali Nabri.
Hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa watu mashuhuri uliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ilihudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali , akiwemo Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Biseko Chiganga, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Musa Mbura pamoja na maofisa kutoka nchi zote mbili.
Isome: EAC yatakiwa kurahisisha usafiri wa anga
Azma ya kufungulia masoko kwa mashirika ya ndege ya Tanzania kwenda Oman ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia ziara yake ya kikazi nchini Oman na utekelezaji wa kampeni ya Royal Tour.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Prof. Mbarawa amesema mkataba wa awali ulisainiwa mwaka 1982, hivyo maboresho yalikuwa ni muhimu, mkataba huu sasa utafungua fursa mpya za usafiri baina ya nchi mbili hizi, kuleta ongezeko la abiria pamoja na kukuza biashara na uchumi.
View this post on Instagram
Kwa upande wake Rais wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga wa nchi hiyo Mhandisi Ali Nabri, alisema hafla hiyo ni sehemu muhimu sana siyo tu katika kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania na Oman, bali ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa nchi zote mbili.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga ambaye alisema kazi iliyobaki sasa ni kuanza utekelezaji na amesisitiza kuwa TCAA imejipanga kuhakikisha inashirikiana na wadau wengine, ili kuendelea kuboresha mazingira katika sekta ya usafiri wa anga nchini na kuufanya uwe chachu ya maendeleo.



