Samia atuma salamu za pole kifo cha Odinga
RAIS Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa watu wa Kenya kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga kilichotokea India akiwa na umri wa miaka 80.
Familia yake imesema amefariki dunia leo asubuhi kwa mshituko wa moyo wakati wa mazoezi ya kutembea katika hospitali ya Ayurvedic iliyopo Manispaa ya Koothattukulam Jimbo la Kerala.
SOMA; Odinga atoa msimamo uamuzi wa mahakama
Kupitia mitandao yake rasmi ya kiajamii Rais Samia amesema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto, Mama Ida Odinga, watoto, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Kenya kwa msiba huu.
Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki, na ailaze roho ya mpendwa wetu, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, mahali pema peponi.”



