Mkazi wa Kimara aeleza Vicoba ‘ilivyouza’ nyumba yake kimakosa

MKAZI wa Kimara, Sara Mtoka ameeleza namna kikundi cha kukopeshana fedha cha wanawake (VICOBA) kilivyosababisha nyumba yake kuuzwa kimakosa.
Mtoka alieleza hayo jana Mbagala alipofika kwenye Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa ajili ya kupata msaada wa kurejeshewa nyumba yake.
Alidai mwaka 2012 alikuwa amejiunga na kikundi cha akinamama ambacho walikuwa wakishirikiana na kusaidiana, kukopesha na kukuza biashara zao.
Alieleza kuwa siku moja, mmoja wao aliwafahamisha kwamba anahitaji kudhaminiwa kwa ajili ya mkopo. Kwa kuwa walikuwa wanaaminiana, walimdhamini.
“Bila sisi kujua, mwenzetu aliwasilisha leseni zetu za makazi kwa Kampuni moja inayoitwa Giant. Kampuni hiyo iliweza kutumia leseni hizo kuingia mkataba wa mnada, bila sisi kuweka saini sehemu yoyote. Baadaye tukagundua nyumba zetu zimeuzwa. Mwenzetu aliyedai kupata mkopo alitumia majina yetu na akachukua zaidi ya Shilingi milioni 20 badala ya milioni 10 alizotuambia,” alisimulia Mtoka.
Alisimulia kuwa nyumba yake iliwekwa mnada akiwa safarini na binti yake ndiye aliyeitwa na kushinikizwa kutia saini.
Alieleza kuwa baada ya kurejea, alifungua kesi katika Mahakama ya Ardhi na kushinda.
Hata hivyo, mnunuzi wa nyumba aliendelea kudai kuwa yeye ni mmiliki halali na akawasilisha hati ya makazi ili asiondolewe kwenye nyumba.
Alisema hakuwa na mwanasheria bali alibahatika kupata wakili aliyemsaidia kupeleka kesi yake Mahakama Kuu ambapo mwaka 2022 alishinda lakini ili hukumu itekelezwe, ilibidi awalipe madalali wa mahakama Sh milioni sita ili waondoe wapangaji waliopo kwenye nyumba hiyo.
“Mimi sina uwezo huo bado nalipa kodi, nasomesha watoto wangu, mmoja yuko chuo na biashara zangu ni ndogo kama zilivyo kwa akinamama wengi,” alisema.
Alisema aliposikia kampeni hiyo aliamua kwenda kuuliza iwapo kuna namna ya kusaidiwa. “Nashukuru sana wameelewa shida yangu, wamechukua vielelezo vyangu na wamesema watafuatilia kwa karibu mimi pia nitaendelea kufuatilia kwa matumaini makubwa,” alisema.