Mke, mume washikiliwa kwa kuwachoma moto watoto wao

JESHI la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia Yohana Josephat (40) na mkewe, Lucia Michael (30), wakazi wa Busega kwa kosa la kuwajeruhi watoto wao kwa kuwachoma moto sehemu mbalimbali za miili yao wakiwatuhumu kuiba mahindi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Blasius Chatanda, tukio hilo lilijiri Julai 29, mwaka huu, katika Kijiji cha Yitwimila wilayani Busega mkoani Simiyu, chanzo kikitajwa kuwa ni watoto hao kuiba ndoo ya mahindi nyumbani kwa bibi yao ndipo wazazi wakaamua kuwaadhibu kwa kuwachoma moto.

Chatanda alisema wazazi hao waliamua kuwachoma moto watoto wao maeneo mbalimbali ya mwili na kwamba adhabu hiyo ni kubwa na hatarishi.

Alisema kwa sasa watoto hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Nassa kilichopo wilayani humo.

Wakizungumza wakiwa katika kituo cha afya Nassa wanapopatiwa matibabu watoto hao, wameeleza namna walivyoadhibiwa baada ya kubainika kuchukua mahindi na kuyauza na walisema kuwa waliyauza ili waweze kujipatia mahitaji yao ya msingi.

Dk Sally Shau anayewatibu watoto hao alisema hali zao zimeanza kuimarika.

Aidha, Kamanda Chatanda, mbali na kuhimiza wazazi kuacha kujichukulia sheria mikononi, alisema wanandoa hao watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button