WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kuimarisha ushirikiano kati yao, viwanda na wabunifu au wazalishaji ili kufanikisha maendeleo katika sekta ya nguo na mavazi.
Waziri Mkenda ametoa maagizo hayo leo Machi 15 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kongamano la kujadili maendeleo na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ambapo amesema ushirikiano huo utawajengea uwezo vijana na wabunifu katika kuhakikisha wanapata ujuzi stahiki unaohitajika kwenye soko la ajira na viwandani.

Amesema asilimia kubwa ya wanaojihusisha katika sekta hiyo hawana kiwango kikubwa cha elimu lakini wana ujuzi na ubunifu mzuri katika kutengeneza bidhaa zinazovutia.
“Nawapa jukumu VETA mkaongeze ushirikiano baina yenu, wamiliki wa viwanda na wabunifu wa mavazi na nguo, kuwajengea uwezo vijana wetu ambao wapo vyuoni wanapata kupewa ujuzi halisi wa kusaidia sekta hiyo,” amesema Mkenda.

Waziri huyo ameongeza kuwa uwepo wa Vyuo vya Ufundi Stadi nchini vimesaidia katika kukuza ujuzi na kuwawezesha wananchi kujiajiri na kuajiriwa, na kwamba Serikali imejizatiti kujenga na kuimarisha vyuo hivyo.