Mkumbo ataka stendi ya Katesh ikamilike kwa wakati

MANYARA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametoa maagizo kwa mkandarasi anayejenga stendi mpya ya mabasi ya Katesh kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Prof Mkumbo amesema hayo alipoweka Jiwe la Msingi la stendi hiyo inayojulikana kama Stendi ya Dk Samia Suluhu Hassan wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Aidha, prof Mkumbo alisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kurahisisha huduma za usafiri na kukuza biashara za wananchi.

Mradi huo una thamani ya Sh bilioni 5.69, ukigharimiwa kikamilifu na serikali ya awamu ya sita.

Prof Mkumbo alisema kuwa lengo la Serikali ni kuboresha maisha ya wananchi kwa kubuni miradi inayorahisisha upatikanaji wa huduma muhimu.

“Mradi huu mkubwa utawanufaisha akina mama na vijana, ambao wanapaswa kupewa kipaumbele katika nafasi za biashara zitakazotokana na stendi hii,” aliongeza prof Mkumbo. 

Mbunge wa Jimbo la Hanang, Mhandisi Samwel Hhayuma alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto kubwa za jamii, ikiwemo maji, afya, elimu, na miundombinu ya barabara.

Hhayuma alisema maendeleo yanayoonekana sasa ni matokeo ya juhudi thabiti za serikali ya awamu ya Sita.

Stendi hiyo mpya inajengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 5.88, na kazi inatekelezwa na mkandarasi mzawa, Elerai Construction Company Limited, huku usimamizi wa kitaalamu ukifanywa na Bureau for Industrial Cooperation (BICO) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hadi sasa mradi umefikia asilimia 85 ya utekelezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay stendi hiyo itakuwa na majengo ya kisasa, ikiwemo jengo lenye ghorofa moja kwa ajili ya abiria kusubiri mabasi, ofisi za utawala, na majengo matatu yenye vyumba 90 vya maduka.

Katika ziara hiyo, prof Mkumbo pia alitembelea Shule ya Sekondari ya Mulbadaw ambako alizindua mradi wa miundombinu ya maabara za masomo ya sayansi na kukagua madarasa na mabweni, akisisitiza umuhimu wa walimu wa kilimo kufundisha katika shule hiyo ili kukuza ujuzi wa wanafunzi katika sekta ya kilimo.

Habari Zifananazo

Back to top button