Mkutano wa petroli Afrika Mashariki kufanyika Dar es Salaam

KONGAMANO la Mkutano wa 11 wa Afrika Mashariki la Petroli (EAPCE 2025) linatarajiwa kufanyika Machi 5-7 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felician Mramba amesema maandalizi yote kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika na kama taifa wanatarajia kunufaika pakubwa kutokana na kupata elimu kutoka kwa wataalamu mbalimbali.
“Mkutano wetu tunatarajia utafunguliwa na Rais Samia Saluhu Hassan na kuna fursa nyingi za kibiashara na uwekezaji hasa kwenye sekta ya nishati, lengo letu ni kutaka Afrika Mashariki kutumia nishati safi na kuachana na matumizi ya mkaa,” amesema Mramba.
Mramba amesema kongamano hilo litahudhuriwa na wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania na pia kutakuwa na maonesho ya mbalimbali biashara za kiasili ambazo zitajumuisha wafanyabiasharai zaidi ya 1,000 wanaotarajiwa kuhudhuria.
Kiongozi huyo amewaomba wafanyabiashara mbalimbali kutumia fursa hiyo kujitokeza kuwekeza na kutangaza biashara zao kupitia kongamano hilo.
Kwa upande wake mwakilishi wa EAPCE, kutoka nchini Rwanda, Jean Baptisti alisema umuhimu wa Kongamano hilo ni kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki na kueneza matumizi ya nishati mijini na vijijini kwa nchi zote wanachama.
Naye Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, James Matarajio, amesema kongamano hilo hufanyika kila baada ya miaka miwili na hufanyika kwa mzunguko kwa kuhusisha nchi wanachama.



