Mkutano wa pili wa nyuklia kufanyika Italia

ROME : VIONGOZI wa Ghuba na Mashariki ya Kati wameanza ziara katika mataifa mbalimbali kabla ya mkutano wa pili wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran, itakayofanyika Jumamosi mjini Roma.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, pamoja na Kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, wamewasili Moscow kwa ajili ya kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin. Kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Khalid bin Salman, anatarajiwa kutembelea Tehran.
SOMA: Marekani , Iran kujadili mpango wa nyuklia
Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran ilifanyika Muscat, Oman, wakati ambapo Rais Donald Trump na Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, walikuwa wakibadilishana maneno makali na vitisho. Mazungumzo haya yamekuja katika kipindi cha mvutano mkubwa kati ya mataifa haya.
Hata hivyo, inatarajiwa kwamba mazungumzo haya yatakuwa magumu, kwani Iran inasisitiza kwamba haki yake ya kurutubisha madini ya urani haiwezi kuwa sehemu ya majadiliano. Hali hii inatoa changamoto kubwa kwa pande zote katika kutafuta muafaka wa kudumu.



