Mkuu wa Magereza awataka watumishi kutohofu kustaafu

DODOMA: MKUU wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Jeremiah Katungu amewataka watumishi kutokuwa na hofu ya kustaafu. Alisema hayo juzi wakati wa sherehe ya kuwaaga wastaafu 28 wa Jeshi la Magereza iliyofanyika Msalato jijini Dodoma.

“Acheni kuwa na hofu ya kustaafu kwani baada ya kustaafu maisha lazima yaendelee, jambo la muhimu ni kujipanga kuishi maisha baada ya kustaafu,” alisema.

Pia, alisema kustaafu kwa heshima ni muhimu katika utumishi wa umma kwani ni kuacha alama kwa kujitoa kwao kushiriki katika shughuli mbalimbali za jeshi.

“Mmeandika historia kubwa, kuna mmoja kati yenu katumikia serikali miaka 41, hili ni jambo kubwa sana, kuna waliotamani kufikia hatua hii lakini kwa sababu mbalimbali hawakuweza kufanikiwa, jambo hili ni la kumshukuru Mungu,” alisema.

Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza pia aliwataka watumishi wa jeshi hilo kuendelea kufanya kazi na kujituma na kuenzi mazuri yaliyofanywa na watumishi ambao wamestaafu.

“Nasisitiza suala la umoja, kuwa na mwelekeo katika kudumisha mshikamano na kulipa heshima jeshi mbele ya serikali na jamii,” alisema.

Alisema milango iko wazi wakati wote kutoka kwa wastaafu hao na watapokea maoni na ushauri ili kuhakikisha jeshi linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, alihimiza kudumisha umoja na mshikamano ili kuilinda amani ya nchi.

“Tuendelea kushirikiana kuilinda amani ya nchi,” alisema. Akizungumza kwa niaba ya wastaafu, Kamishna mstaafu Bertha Minde alishukuru jeshi hilo kwa kukubali kuwaaga na kuwapatia zawadi. “Sisi tayari ni wastaafu, waliopo tunawaomba muendelee kufanya kazi kwa umoja, sisi licha ya kuondoka tutaendelea kuwa jicho la jeshi,” alisema.

Alipongeza jeshi hilo kwa kufanya kazi kwa kutumia mifumo badala ya kutumia mafaili kama ilivyokuwa awali na pia kujikita katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye magereza yote nchini. Aliwataka watumishi kuwa na nidhamu ili kuwezesha jeshi hilo kufika mahali panapotakiwa.

Aliwahimiza wastaafu kujipanga ili kuishi maisha ya uraiani baada ya utumishi wao wa kutumikia taifa. Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mariam Mbaga aliwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi kwani mchango wao ni muhimu kwenye taifa.

“Tuendelee kushirikiana pia kutenga muda kushiriki matukio mbalimbali ya kijamii ili kuimarisha mshikamano,” alisema. Awali, wakati wa kuaga wastaafu hao, Kamishna mstaafu Bertha Minde alipanda gari maalumu lililokuwa likisindikizwa na maofisa sita wa jeshi hilo kama ishara ya kumaliza muda wa kutumikia jeshi hilo. Kamishna huyo mstaafu ametumikia jeshi hilo miaka 34.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button