Kampuni kununua kilo milioni 265 za tumbaku

KAMPUNI ya Mkwawa Leaf Tobacco Ltd imeahidi kununua kilo milioni 265 za tumbaku katika misimu mitatu ya soko hatua inayotarajiwa kupeleka furaha kwa wakulima na kusaidia kuongeza tija katika kilimo cha zao hilo nchini.

Mmiliki wa kampuni hiyo, Ahamed Huwel alisema katika msimu huu kampuni hiyo ina mikataba ya kununua kilo milioni 45 huku kilo milioni 90 zikitarajiwa kununuliwa msimu unaofuta na kilo milioni 130 msimu wa tatu.

Alitoa taarifa hiyo katika hafla ya ufunguzi wa msimu wa masoko ya tumbaku wa msimu huu wa 2023/2024 uliofanyika katika Chama cha Msingi Nsimbo wilayani Nsimbo mkoani Katavi.

Uzinduzi wa masoko hayo uliosindikizwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii mbalimbali maarufu akiwemo Zuchu, Baba Levo na wengineo.

Huwel alisema tumbaku hiyo itanunuliwa kupitia sera yao ya ‘Lima kwa Kadri ya Uwezo Wako’ inayolenga kuchochea uzalishaji wa zao hilo la biashara katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mkwawa ilipoingia katika biashara hii ilikuta wakulima wakilima kwa kuzingatia makisio ya masoko lakini sisi tumeondoa utaratibu huo kwa kuwa tuna soko kubwa na la uhakika ndio maana tunawahamasisha wakulima kulima kwa kadri ya uwezo wao kwani soko lipo,” alisema.

Alisikitika hasara wanayopata wakulima wa Nsimbo akisema utafiti waliofanya na timu yake ya wataalamu inaonesha katika kila ekari moja inayotoa wastani wa kilo 1,000 za tumbaku kila mkulima amekuwa akipoteza wastani wa kilo 450 hadi 500 ambayo ni hasara ya zaidi ya Sh Milioni 1.9.

“Na kwa ekari 2,500 za tumbaku zilizoko katika jimbo hili la Nsimbo, hesabu zetu zinaonesha wakulima kwa ujumla wake wamekuwa wakipoteza zaidi ya Sh Bilioni 5 kwasababu ya usimamizi mbovu wa uzalishaji wa zao hilo,”alisema.

Alisema kampuni yake ambayo ni kampuni ya kitanzania imeingia katika biashara hiyo kwa nguvu na kwa kuzingatia taratibu zote zitakazowezesha mipango ya serikali kwa kupitia maelekeo ya Ilani ya CCM kutengeneza mazingira yatakayowezesha tani 250,000 za zao hilo zinazalishwa nchini kote ifikapo mwaka 2025.

“Tumejipanga vizuri sana, mimi kama kampuni ya Mkwawa sitalala katika azma yetu ya kuwainua wakulima vinginevyo ni bora nilaanike nisifanye biashara hii,” alisema.

Akizungumzia hila zinazofanywa na baadhi ya wanunuzi wa zao hilo, Huwel aliziomba mamlaka zinazosimamia kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za maeneo husika ukiwemo mkoa wa Mbeya na Katavi kukomesha ukiukwaji wa mikataba.

“Kama wakulima hawa wataona Mkwawa anawafaa basi waendelee kuwa na Mkwawa na kama wataona hawamfai wana haki ya kumfukuza na kumtafuta mtu mwingine kwa kuzingatia taratibu. Katika mikoa ya Katavi na Mbeya kuna vitu katika ununuzi wa zao hilo vinatendeka ambavyo haviko sawa,” alisema.

Akizindua soko hilo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliipongeza kampuni hiyo kwa kuwa moja ya makampuni makubwa yanayonunua zao akisema kilimo cha Tumbaku kina faida kwa wananchi na ni moja ya mazao yanayoliingizia taifa fedha nyingi zikiwemo za kigeni.

Alisema serikali imeiamini kampuni hiyo na akata wautumie uaminifu waliopewa kuhakikisha mkulima na wahusika wengine wote katika sekta hiyo wanapata haki zao kwa mujibu wa kanuni, taratibu, miongozo na sheria.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo, Salum Maduhu alisema tangu kampuni hiyo ianze kufanya kazi wana matumaini makubwa na soko la zao hilo na kilimo chao kinatarajiwa kuongezeka.

Mbunge wa jimbo la Nsimbo, Annah Lupembe amewataka viongozi kuwaacha wakulima wamchague mnunuzi wanayemtaka akisema baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro kwasababu wamekuwa wakiingilia uchaguzi wa wanunuzi.

“Tuwaache wakulima wajichagulie mnunuzi wao wenyewe kwani wao ndio wanaohangaika na kuteseka na jua na mvua katika mashamba yao, sio sawa kuwaingilia kwenye maamuzi yao,” alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) Said Ntahondi ameishukuru serikali kwa kuileta Kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco Ltd akisema inaonesha kwa vitendo dhamira ya kufufua na kuchochea uzalishaji wa zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati huo huo, kampuni hiyo ya Mkwawa Leaf Tobacco Ltd imeahidi kuchimba visima vya maji katika vijiji vyote vya jimbo la Nsimbo kama moja ya mipango yake ya kurudisha kwa wananchi kile inachopata kutoka katika biashara ya zao hilo na kuunga mkono juhudi za mbunge wa jimbo hilo zinazolenga kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x